Fahamu madhara ya kukata kimeo au kilimi

0
4

Kimeo kinachojulikana pia kama kilimi ama kitaalamu kama uvula, ni sehemu ndogo ya nyama inayoning’inia nyuma ya koo kwenye sehemu ya juu ya kinywa.

Faida za kimeo

Husaidia kumeza
Wakati wa kumeza, kimeo husaidia kuzuia chakula na vinywaji visiingie kwenye njia ya hewa kwa kusaidia kufunga njia inayoelekea kwenye pua. Kimeo huchangia katika uzalishaji wa ute (mucus) unaosaidia kulainisha koo na kinywa, hivyo kuwezesha kumeza chakula kwa urahisi.

Kinga ya mwili
Kimeo kina seli za kinga ambazo husaidia kuchuja na kuzuia viumbe hatarishi kama bakteria na virusi kuingia mwilini kupitia njia ya hewa au chakula.

Utamkaji wa sauti
Kimeo husaidia katika kutengeneza sauti fulani wakati wa kuzungumza, hivyo kuchangia katika utoaji wa matamshi sahihi.

Madhara ya kukata kimeo

Ingawa katika baadhi ya jamii kuna imani kwamba kukata kimeo ni suluhisho la matatizo kama kikohozi sugu au matatizo mengine ya koo, wataalamu wa afya wanatahadharisha dhidi ya utaratibu huu kutokana na madhara yafuatayo:

Kutokwa na damu nyingi
Kukata kimeo kunaweza kusababisha kutokwa na damu nyingi, ambayo inaweza kuhatarisha maisha hasa kwa watoto wachanga.

Maambukizi
Matumizi ya vifaa visivyo safi au mazingira yasiyo ya usafi wakati wa kukata kimeo yanaweza kusababisha maambukizi ya bakteria, ambayo yanaweza kuathiri afya kwa ujumla.

Matatizo ya kumeza na kuongea
Kama ilivyoelezwa awali, kimeo kinasaidia katika kumeza na na upande wa sauti. Kukiondoa kunaweza kusababisha matatizo katika kumeza na kuzungumza.

Kifo
Katika baadhi ya matukio, watoto wamepoteza maisha kutokana na madhara ya kukatwa kimeo, kama vile kutokwa na damu nyingi au maambukizi makali.

Ukataji wa kimeo unaweza kuhusishwa na mtaalamu wa afya pale tu kunapokuwa na sababu za kiafya zilizothibitishwa. Sababu zinazoweza kumfanya daktari kupendekeza kukatwa kwa kimeo ni pamoja na:

Uvimbaji wa kimeo (Uvulitis)
Hii ni hali ambapo kimeo kinaweza kuvimba na kuwa kikubwa zaidi, hali inayoweza kusababisha matatizo ya kupumua, kumeza, au kuongea. Endapo matibabu ya kawaida hayafanyi kazi, upasuaji wa kuondoa kimeo unaweza kuzingatiwa.

Matatizo ya kupumua wakati wa usingizi (Sleep Apnea)
Kwa baadhi ya watu, kimeo kikubwa kinaweza kuziba njia ya hewa wakati wa usingizi, na hivyo kuchangia tatizo la kupumua linalojulikana kama sleep apnea. Katika hali kama hizi, kuondoa kimeo kunaweza kusaidia kuboresha mtiririko wa hewa.

Maambukizi ya mara kwa mara
Ikiwa mtu anapata maambukizi ya mara kwa mara kwenye eneo la kimeo ambayo yameshindwa kudhibitiwa kwa dawa, daktari anaweza kupendekeza kuondoa kimeo ili kuzuia maambukizi zaidi.

Kimeo ni sehemu muhimu ya mwili na hakipaswi kukatwa bila sababu za kiafya zilizothibitishwa na mtaalamu wa afya. Iwapo mtu anakabiliwa na matatizo kama kikohozi sugu au dalili nyingine zisizoeleweka, ni vyema kutafuta ushauri wa daktari badala ya kutumia njia za kienyeji ambazo zinaweza kuwa na madhara makubwa.

Send this to a friend