Fahamu majukumu ya Jaji Kiongozi na kesi anazopaswa kusikiliza

0
40

Oktoba 8 mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan alimteua Jaji Mustapha Siyani kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu nchini Tanzania, kushika nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Elieza Feleshi, ambaye sasa amekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kabla ya uteuzi huo Jaji Siyani ambaye ndiye aliyekuwa akisikiliza kesi ya uhujumu uchumi namba 16/2021 inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu, alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.

Mapema leo baada ya kutoa uamuzi mdogo katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa inayowakabili watuhumiwa hao, Jaji Siyani aliitangaza kujitoa kwenye kesi hiyo kwa kile alichosema kuwa majukumu aliyonayo yanaweza kumchelewesha kuiepeleka kesi kwa haraka.

Je Jaji Kiongozi anaweza kuendesha kesi?

Katika mahojiano na Gazeti la Mwananchi Wakili Timon Vitalis amesema Jaji Kiongozi ana mamlaka ya kusikiliza mashauri yote ya Mahakama Kuu kama ilivyo kwa jaji yoyote wa Mahakama Kuu.

“Ndio maana ulikuwa unaona Jaji Kiongozi alikuwa anasikiliza kesi ya mauaji iliyokuwa inamkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe na wenzake 12, Jaji Kiongozi wa wakati ule Salum Masati alikuwa anasikiliza kesi ile. Nakumbuka kesi ya Zombe ilifunguliwa katika masjala ya kawaida na sio Masjala Kuu, lakini ilisikilizwa na Jaji Kiongozi,” amesema Vitalis.

Kwa upande wake, Wakili Francis Stolla amesema kama kutakuwa na maelekezo kutoka juu yakatolewa na Jaji Mkuu anaweza akasema Jaji Kiongozi akaendeshe kesi kama Jaji wa kawaida.

Kuhusu majukumu ya Jaji Kiongozi, Ibara ya 109 (3) hadi (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kuwa Jaji Kiongozi ni Msaidizi wa Jaji Mkuu katika kusimamia Mahakama Kuu na mahakama zote za chini.

Kwa upande wake Stolla amesema, “Kwanza Jaji Kiongozi ana majukumu ya jaji wa kawaida wa Mahakama Kuu, yaani yeye ni Jaji wa Mahakama Kuu kwa hiyo anafanya kazi ambazo Jaji wa Mahakama Kuu yeyote yule anafaya.

“Jukumu lake la pili kwa kuwa yeye ni Jaji Kiongozi maana yake anaongoza Mahakama Kuu, yaani majaji wote wa Mahakama Kuu yeye ndio kiongozi wao.”

Jukumu la tatu la Jaji Kiongozi ambaye mbali ya kuwa msimamizi wa Masjala Kuu, pia ni msaidizi wa Jaji Mkuu wa Tanzania katika kuongoza Mahakama Kuu, kwa maana kwamba Mahakama Kuu pia inaongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania.

Chanzo: Mwananchi

 

Send this to a friend