Fahamu sababu za viwanja vya ndege kujengwa karibu na bahari/maziwa

0
46

Mioyo ya Watanzania bado ingalia imejawa na majonzi kuhusu vifo vya wenzao 19 vilivyotokana na ajali ya dege ya Precision Air mkoani Kagera iliyopata ajali katika Ziwa Victoria, maswali yamekuwa mengi, na moja ya hayo ni lile linalohoji sababu za viwanja vya ndege kujengwa pembezoni mwa vyanzo vya maji.

Hili si jambo geni, tangu awali, viwanja vya ndege vilijengwa katika miji mikubwa, na miji mikubwa ilikuwa karibu na maji kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi ambapo bidhaa nyingi zilisafirishwa kwa njia ya meli kutokana na kutokuwepo kwa treni au barabara zilizounganisha kila kona ya nchi.

Mahitaji makubwa ya usafiri yalipelekea viwanja vya ndege kuhitajika zaidi, lakini hiyo sio sababu pekee ya viwanja hivyo kujengwa karibu na maji.

Hizi ni sababu za kwanini viwanja vya ndege hujengwa karibu na maji;

Kuzuia kelele
Watu waishio karibu na viwanja vya ndege ni wazi hawapendi kusumbuliwa na injini za ndege haswa nyakati za usiku. Wakati wa kupaa na kutua, ndege huruka kwa mwinuko wa chini ambao unaweza kusababisha kelele kubwa, hivyo kupita juu ya maji kabla ya kufikia miinuko fulani husaidia kupunguza kelele katika maeneo ya watu.

Waziri Mbarawa: Wakati ajali ya ndege inatokea, boti ya uokoaji ilikuwa mbali

Sababu za kiusalama
Wakati mwingine rubani huenda asiweze kutua kwa usahihi au kupaa, badala ya kuelekeza ndege kwenye jengo, ardini au kwingine, marubani wanaweza kuielekeza kwenye hivyo kupunguza makali ya madhara ambayo yangeweza kutokea endapo ndege ingetua nchi kavu.

Kuepusha vizuizi
Ndege pia haziwezi kukutana na vizuizi vyovyote kama miti, majengo au nyaya za umeme wakati wa kutua. Juu ya maji hakuna kitakachozuia ndege kuruka au kutua, hivyo huifanya kuwa salama zaidi.

Madhara ya kujenga viwanja vya ndege kando kando ya maji;

Upepo
Kujenga viwanja vya ndege karibu na maji bado kuna hasara zake. Upepo kwa kawaida huwa na nguvu karibu na sehemu za maji kutokana na ukosefu wa vizuia upepo.

Mafuriko
Viwanja vya ndege vilivyo karibu na vyanzo vya maji vinahitaji kulindwa dhidi ya mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa au hali ya hewa ya dhoruba. Uwanja wa ndege wa Kansai nchini Japan ulifurika Septemba 2018 kutokana na kimbunga hivyo kulazimika kusimamisha shughuli kwa siku 2 kutokana na maji kuwa mengi.

Ukungu
Wakati wa vuli na baridi, maeneo ya pwani yanakabiliwa na ukungu. Ukungu hutokea wakati hewa yenye joto na unyevu inaposonga juu ya ardhi yenye baridi kiasi. Ukungu wa aina hii huitwa ‘advection fog’ na hupatikana sana karibu na mikondo ya bahari yenye joto katika hali ya hewa ya baridi. Uwepo wa ukungu huweza kuwa changamoto kwa ndege kutua au kuruka.

Je! Wewe unadhani kwanini viwanja hujengwa karibu na maziwa, mito au bahari?