
Matumizi ya mitandao imeongezeka kwa kasi ulimwenguni ambapo huduma mbalimbali zimerahisishwa. Ongezeko hilo linakwenda sambamba na ongezeko la wizi na utapeli, ambapo walaghai hutumia njia mbalimbali kufanikisha uhalifu wao.
Ili kuepuka kuwa miongoni mwa waathirika hao, fuatilia mbinu hizi zinazotumika kulaghai watu mitandaoni;
Ahadi za faida kubwa pasipo juhudi
Moja ya dalili kubwa za utapeli ni ujumbe unaodai unaweza kupata pesa nyingi kwa muda mfupi bila kufanya kazi kubwa. Mara nyingi huahidi faida ya haraka na fursa ya kipekee ambayo haihitaji uzoefu.
Ujumbe wa dharura au wa vitisho
Walaghai hutuma ujumbe unaosema akaunti yako itafungwa, simu itakatwa au una deni fulani. Lengo ni kukuogopesha ili uchukue hatua haraka bila kuchunguza ukweli.
Kuombwa taarifa binafsi au za siri
Hakuna taasisi halali inayokuomba namba ya siri, OTP, PIN ya benki au taarifa za kitambulisho kupitia ujumbe au simu. Ombi la aina hii ni ishara wazi ya utapeli.
Viungio (links) na tovuti za kutia shaka
Ujumbe wenye link zisizoeleweka au tovuti zinazofanana na rasmi lakini zina herufi chache tofauti ni hatari. Walaghai hutengeneza tovuti bandia ili kukuibia taarifa zako.
Makosa mengi ya lugha
Ujumbe kutoka kwa taasisi kubwa ukiwa na makosa mengi ya kisarufi, lugha isiyo rasmi au maneno yasiyoeleweka vizuri mara nyingi huwa wa utapeli.
Kushinikizwa kufanya uamuzi wa haraka
Matapeli hukulazimisha ufanye uamuzi papo hapo wakisema ofa inaisha leo au pesa zitapotea. Lengo ni kukunyima muda wa kufikiri au kutafuta ushauri.
Ombi la kutuma pesa kabla ya huduma
Kuombwa utume fedha ili upate kazi, mkopo, zawadi, msaada au kujiunga na mradi fulani ni dalili ya utapeli. Huduma halali hazihitaji malipo ya awali yasiyo na uthibitisho.
Akaunti bandia au zisizo na taarifa kamili
Akaunti mpya zisizo na picha halisi, anwani, maelezo ya mawasiliano au uthibitisho wa kisheria ni hatari. Wengine hujifanya kuwa watu maarufu au taasisi za serikali.
Ahadi za zawadi au ushindi usiohusika
Kupokea ujumbe kuwa umeshinda bahati nasibu au zawadi bila kushiriki ni utapeli. Walaghai hutumia zawadi za uongo kuwavutia waathirika.
Kuwasiliana kwa siri
Walaghai hukataa kukutana ana kwa ana, kutoa anwani halisi au kutumia barua pepe na namba rasmi. Mara nyingi wanataka mawasiliano yaendelee kwa siri.







