Mkuu wa mkoa wa Iringa, Queen Sendiga amepiga marufuku wananchi wote kutupa takataka na kuchafua mazingira hovyo ili kuendelea kuyaweka mazingira kuwa masafi na na kuepuka kukumbana na magonjwa ya mlipuko.
Akizungumza mara baada ya kumaliza kufanya usafi kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo, Sendiga amesema mkoa wa huo umekuwa na sifa ya kufanya vizuri kwenye suala la usafi hivyo wanapaswa kuendelea kufanya usafi na kuyaweka mazingira safi.
Sendiga amesema kuwa lengo lake ni kuhakikisha mkoa wa Iringa unashika namba moja kwa kuwa na mazingira bora na masafi na kuongoza kwa usafi kitaifa kama ambavyo ilikuwa miaka ya nyuma.
Kwa upande wake afisa mazingira wa Manispaa ya Iringa, Abdon Mapunda amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu ya usafi kwa wananchi wote ili wajue umhimu wa kutunza mazingira yanayowazunguka.
Mapunda amesema mwananchi akikamatwa ametupa takataka hovyo na kuchafua mazingira atatozwa faini ya shilingi 50,000, huku lengo likiwa kuhakikisha wananchi wanajifunza namna bora ya utunzaji wa mazingira.