Falme za Kiarabu kuipatia Tanzania mkopo wa TZS bilioni 978

0
38

Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi wa Umoja wa Falme za Kiarabu umeahidi kutoa mkopo nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania ukiwemo Mradi wa Umeme wa Benaco-Kyaka, mkoani Kagera na ujenzi wa makazi ya watumishi ya gharama nafuu visiwani Zanzibar, inayokadiriwa kugharimu dola za Kimarekani milioni 420 [sawa na TZS bilioni 978.6].

Ahadi hiyo imetolewa Mjini Abu Dhabi na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund for Development), Mohammed Saif Al Suwaidi, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, makao makuu ya mfuko huo mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mkurugenzi huyo amemweleza Dkt. Nchemba kuwa miradi mingine ya kimkakati iliyowasilishwa na Serikali ya Tanzania kwenye mfuko huo ukiwemo wa Ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere na Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) itatafutiwa ufadhili kupitia Serikali pamoja na Sekta binafsi ya nchi hizo kwa kuwa inahitaji uwekezaji mkubwa wa fedha.

Aidha, amesema mfuko wake uko tayari kusaidia pia utekelezaji wa miradi mingine ya kilimo na uvuvi kupitia kampuni inayojishughulisha na masuala hayo katika Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Aidha, Dkt. Nchemba, ameushukuru mfuko huo kwa kutoa fedha kiasi cha Shilingi milioni 201 na dola za Marekani milioni 1.3 [sawa na TZS bilioni 3] kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa barabara ya Uvinza-Ilunde hadi Malagarasi yenye urefu wa kilometa 51.1 kwa kiwango cha lami, barabara ambayo ujenzi wake umerejea baada ya kukwama kwa muda mrefu.

Send this to a friend