Fedha za TRAB na TRAT si za Serikali 

0
26

Serikali imesema inajenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara kwa kutotumia fedha zilizopo kwenye mashauri yanayobishaniwa katika Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) na Baraza la Rufaa za Kodi (TRAT) ili kutoa haki kupitia vyombo hivyo vinavyoongozwa na wanasheria mahiri.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalam, Janejelly James, aliyetaka kujua muda ambao Serikali itamaliza mashauri ya kikodi yaliyopo TRAT na TRAB ili fedha zilizopo huko zirudi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kufanya kazi za maendeleo pamoja na kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara.

Aidha, Dkt. Nchemba amesema fedha zinazobishaniwa na kabla hazijaamuriwa na vyombo husika haziwi fedha za Serikali, hivyo haziwezi kutumiwa na Serikali katika shughuli zake za maendeleo.

“Serikali ingekuwa inyoosha tu mkono na kusema tunachokadiria sisi ndicho tunataka kilipwe! hiyo ndiyo ingeharibu mahusiano na walipa kodi. Fedha zilizopo TRAB na TRAT zitakuwa fedha za Serikali iwapo vyombo hivyo vitasema sasa hii ni fedha ya Serikali, hilo linafanyika ili kutoa fursa ya haki kutendeka,” amesema Dkt. Nchemba.

Ameongeza kuwa hadi Oktoba 2023, Bodi ya Rufani za Kodi ilikuwa na mashauri 889 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha shilingi trilioni 6.46 na Dola za Kimarekani milioni 4.66 [bilioni 11.7] ambapo katika kipindi hicho, Bodi imesikiliza mashauri 167 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha shilingi trilioni 2.66 na Dola za Kimarekani 201,242.51.

Send this to a friend