Mchezaji mpya wa Azam FC, Feisal Salum (Fei Toto) amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha kuweza kuachana na timu yake ya zamani ya Young African Sports Club na kujiunga rasmi na Azam FC.
Fei Toto amemshukuru Rais Samia leo wakati akisaini mkataba mpya na Azam FC baada ya mvutano wa takribani miezi sita akitaka kuondoka kwenye klabu hiyo bila mafanikio.
“Napenda sana kumshukuru mheshimiwa Rais kwa kufanikisha hili jambo, namtakia kila la kheri kwenye majukumu yake na Mwenyezi Mungu aendelee kumbariki kwa kulimaliza hili jambo.” amesema Fei Toto.
Aidha, ameushukuru uongozi wa klabu hiyo pamoja na mashabiki na kueleza kwamba bado ana mapenzi na klabu hiyo licha ya kuwa ameachana nao rasmi.
Rais Samia awasihi Yanga kumaliza mzozo na Fei Toto
Mei 05, 2023, Rais Samia alitoa wito kwa uongozi wa klabu ya Yanga kutatua changamoto zilizokuwepo baina ya klabu hiyo na Feisal mara alipowaalika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwapongeza kwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF, na kueleza kuwa hafurahishwi kuona hali hiyo iliyokuwa ikiendelea.
“Sifurahii kusikia mnakuwa na mizozo na wachezaji, na sitaki kusema mengi nataka niwaambie kuwa hii issue ya Fei Toto embu kaimalizeni ili tuangalie mbele sasa,” alisema Rais Samia.