Finland yaipa Tanzania heshima ya kipekee Barani Afrika

0
4

Tanzania imetoa wito kwa wawekezaji kutoka nchini Finland kuongeza ushiriki wao katika kuchochea uchumi na biashara nchini kama mbia mkubwa wa maendeleo ya Tanzania.

Hayo yamesemwa na Rais Samia Suluhu wakati akizungumza na waandishi wa Habari pamoja na Rais wa Finland, Alexander Stubb ambaye amewasili nchini kwa ajili ya ziara ya siku tatu kufuatia mwaliko wa Rais Samia Suluhu.

“Kwa muda mrefu Finland imekuwa mbia wetu mkubwa wa maendeleo. Kwahiyo kadri Tanzania inavyokua kiuchumi ni matamanio yetu kuona wawekezaji kutoka nchi rafiki ya Finland wanashirikiana nasi kuchochea biashara na Uchumi,” amesema.

Aidha, Rais Samia amesema katika mazungumzo yaliyofanyika kati ya viongozi hao wawili, Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi mbili pekee barani Afrika ambazo Finland kwa sasa ina ushirikiano wa moja kwa moja wa maendeleo, sambamba na nchi ya Ethiopia.

Mbali na hayo, Rais Samia ameipongeza nchi ya Finland kwa kuendelea kuisaidia Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya usimamizi wa uhifadhi wa mazingira nchini.

Naye, Rais wa Finland, Alexander Stubb ameipongeza Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano wa karibu na taifa hilo, akiongeza zaidi kuwa anaiona Tanzania kama mshirika wake wa karibu wa sasa na siku zijazo.