Forbes yamtaja Rais Samia kuwa mmoja wa Wanawake 100 wenye nguvu zaidi duniani

0
28

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametajwa na jarida la Forbes kama mmoja wa Wanawake 100 wenye nguvu zaidi duniani kwa mwaka 2021.

Orodha hiyo si kwamba inajumuisha wanawake wenye fedha au madaraka, bali mwanamke aliyetumia kipaji chake, sauti au jukwaa kufanya jambo lenye manufaa kwa jamii.

Katika orodha hiyo Rais Samia ameshika nafasi ya 94 ambapo jarida hilo limeeleza namna alivyotumia jukwaa la Mkutano wa Baraza Mkuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kukosoa mgawanyo usio sawa wa chanjo za Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO19).

Alihutumia mkutano huo mkubwa duniani ikiwa ni miezi sita tangu alipoingia madarakani kufuatia kifo cha Rais Dkt. John Magufuli, na alikuwa kiongozi mwanamke wa sita kutoka Afrika kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Forbes imetambua namna Rais Samia alivyotofautisha uongozi wake na wa mtangulizi wake katika mapambano dhidi ya UVIKO19, ambapo ametekeleza hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na karantini ya lazima kwa wageni kutoka nchi zenye aina mpya za virusi.

Nafasi ya kwanza kwenye orodha hiyo yupo MacKezie Scott (mtalaka wa Jeff Bezos) ambaye ni mwanamke watatu kwa utajiri duniani. Wengine ni Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, Melinda Gate, Nancy Pelosi, Spika wa Bunge la Wawakilishi la Marekani.

Wanawake wote 100 wametoka katika nchi 30, katika sekta mbalimbali kama teknolojia, fedha, siasa, burudani, wasaidia jamii, na wote wameunganishwa kutokana na utendaji wao.

Send this to a friend