Gachagua adai wanataka kumuua pamoja na familia yake

0
2

Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, ameibua madai mazito ya njama za kutaka kumuua pamoja na kuwadhuru wanafamilia wake, akimtuhumu Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Douglas Kanja kwa kuhusika moja kwa moja au kwa kufumbia macho vitendo hivyo.

Kupitia barua rasmi aliyoiwasilisha kwa IG Kanja Jumanne, Gachagua amedai kuwa tangu ang’olewe madarakani mwezi Oktoba 2024, amekuwa akilengwa na mashambulizi ya mara kwa mara.

Pia amedai kuwa Mkuu huyo wa Polisi aliondoa walinzi wake kwa makusudi, ili kumuweka katika hatari, akisema ulikuwa ni mpango uliopangwa na watu wabaya wanaoshirikiana na polisi.

Gachagua amedai watu wanaojulikana na IG Kanja wamejaribu kushambulia makazi yake yaliyopo Nairobi, Nyeri, na maeneo mengine. Aidha, mesema maafisa wa Idara ya Ujasusi (NIS) wamekuwa wakimfuatilia yeye na familia yake kwa magari yasiyo na namba za usajili, hali ambayo ameitaja kuwa uvunjaji wa haki yao ya faragha.

Gachagua ameitaka serikali ichukue hatua za haraka kuwalinda raia wote bila upendeleo wowote, huku akisema maisha yake na ya familia yake yako hatarini.