Gachagua amuomba msamaha Ruto kabla bunge halijafanya uamuzi kuhusu hatma yake

0
62

Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua ameomba msamaha kwa Wakenya, bunge na Rais kabla ya wabunge hawajaamua kuhusu kuondolewa kwake ofisini kupitia mchakato wa kumwondoa madarakani.

Gachagua amezungumza wakati wa ibada kanisani kwenye Altari ya Kitaifa ya Maombi jijini Nairobi, akiomba msamaha kwa yeyote aliyeumizwa na maneno au matendo yake akiwa madarakani.

“Nataka kumwambia ndugu yangu Rais William Ruto, kama katika jitihada zetu za kufanya kazi nimekukosea, tafadhali ni samehe kutoka moyoni mwako,” amesema Gachagua.

Gachagua ameendelea kutoa ombi la msamaha kwa wabunge huku akirejelea maneno aliyotoa mwaka 2022 kuhusu ‘wanahisa’ alipoingia madarakani ambapo amesema kuwa nia yake ilikuwa ni kuwashukuru wale waliompigia kura yeye na Rais Ruto, na wala hakukusudia kumkosea yeyote.

“Labda katika kuwashukuru watu wetu na msaada waliotoa kwa Rais na mimi, labda maneno yetu yaliwafanya msijisikie vizuri, hatukukusudia mabaya, tulikuwa tunawashukuru wale waliotupigia kura, kama mnahisi tulikosea, tafadhali sameheni kutoka mioyoni mwenu,” Gachagua aliongeza.

Haya yanajiri katikati ya hoja ya kumwondoa Naibu Rais madarakani iliyowasilishwa bungeni, kwa madai ya utovu wa nidhamu na ukiukaji wa katiba ambapo bunge limemshtumu Gachagua kwa kumdharau Rais Ruto na kujilimbikizia mali kinyume cha sheria tangu alipoingia ofisini, madai ambayo ameyakana.

Send this to a friend