Gachagua: Nilitakiwa kuuawa kwa sumu kabla hoja ya kuondolewa madarakani

0
61

Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amedai kuwa kulikuwa na majaribio mawili ya kumuua kabla ya mashtaka ya kumvua madaraka kuwasilishwa bungeni.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka hospitalini alipokuwa akipatiwa matibabu, Gachagua amesema alikuwa akimwamini sana Rais Wiliam Ruto lakini amekuwa akimsaliti.

“Sijisikii kuwa salama. Tarehe 30 Agosti, maafisa wa polisi wa siri huko Kisumu waliingia chumbani kwangu na mmoja wao alijaribu kuweka sumu kwenye chakula changu, lakini tuligundua hilo na tukafanikiwa kutoroka. Nilipaswa kuuawa kwa sumu.

Tarehe 3 Septemba huko Nyeri, maafisa wa NIS walifika Nyeri na walijaribu kuweka sumu kwenye chakula changu na wazee wa Kikuyu. Niliripoti suala hilo kwa NIS na nikawaomba maafisa waliopangiwa ofisini kwangu waondoke. Baada ya jaribio la kuniua kushindwa, hoja ya kuniondoa iliandaliwa,” amesema Gachagua.

Aidha ameongeza kuwa “Nilimwamini Rais William Ruto, watu wa eneo la Mlima Kenya walimwamini. Tulipokuwa tunajiandaa kuingia madarakani, hakuna mtu mwingine aliyemwamini. Mimi ndiye mtu pekee niliyemwamini kwa maneno kwa sababu sisi ni Wakristo, tulikuwa tunaenda kanisani pamoja. Nilimwamini Mkristo mwenzangu, kwamba hatawasaliti mimi wala watu wangu.”

Gachagua ameendelea kudai kuwa tangu alazwe katika Hospitali ya Karen siku ya Alhamisi, watu wasiojulikana walio karibu na Rais wamekuwa wakipiga simu kuuliza kama hali yake inazidi kuwa mbaya.

“Ninasikia watu wake wengi walikuwa wakipiga simu hapa (hospitalini) wakiuliza kama nimekufa, kama nimepona, kama nitapona, walikuwa wakisherehekea.

Napoiangalia, labda ni historia inajirudia. Rais William Ruto alitaka kunipitisha njia ambayo Rais Moi alimpitisha Matiba. Alimsukuma Matiba hadi kupata kiharusi na kufa. Napoiangalia kile Rais anachonifanyia, hasa sasa wakati nipo hospitalini, akitaka kunidhoofisha, akinitendea kama mnyama [..] Nadhani alitaka kunipitisha njia ya Matiba,” ameeleza.