Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amesema hakuwa sehemu ya maandamano ya vijana dhidi ya serikali yaliyofanyika Juni na Julai mwaka jana.
Akizungumza katika mahojiano, Gachagua ambaye aliondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani Oktoba mwaka jana, amemshutumu aliyekuwa bosi wake, Rais William Ruto kwa kumhusisha na maandamano hayo kama njama ya kumtimua ofisini.
“Vuguvugu la Gen Z lilipoanza, Ruto tayari alikuwa anataka kuniondoa kwenye serikali yake. Aliwaita watu wake na kuwaambia kwamba nilikuwa nikiwahamasisha vijana kwa sababu hakuwa na sababu ya kueleza kwa nini alikuwa ananipiga vita.
Waasi DRC watangaza kusitisha mapigano
“Walishirikiana na kuanza kunishtumu kuwa niliandaa na kufadhili maandamano hayo. Sikufanya hayo yote,” amewaambia wanahabari.
Maandamano hayo yaliyokuwa na vurugu mwaka jana yalimlazimu Rais Ruto kuondoa mswada tata wa fedha uliopendekeza ongezeko la kodi na kuivunja Baraza lake la Mawaziri.
Gachagua, amesema anawaunga mkono kikamilifu vijana wa Kenya, ambao amewataja kuwa nguvu kubwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, huku akiwahimiza kujisajili kama wapiga kura.
Amesema huenda hakuhusika moja kwa moja na maandamano yao, lakini anaunga mkono malengo yao akisema wana ujasiri mkubwa na hawaachi jambo lolote bila kulisemea.