Gambo: Uenyekiti wa Mtaa hauna mshahara, msigombanie mihuri

0
4

Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amewataka wenyeviti wa Serikali za Mtaa watakaoshinda katika uchaguzi, waache mambo ya kugombania mihuri ya Serikali za mtaa kwa ajili ya kujinufaisha kama ambavyo imekuwa ikishuhudiwa kwa baadhi ya wenyeviti wa mitaa na vijiji katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Ameyasema hayo wakati akiwaongoza wanachama na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa katika jimbo lake.

Gambo amesema kazi ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ni kuwaongoza wananchi, kuwasemea, kusikiliza na kutatua kero zao katika maeneo husika na sio kuwafanya kitega uchumi ili wajinufaishe wenyewe kwa kutumia mihuri.

“Sote tunajua kazi ya uenyekiti wa Serikali ya Mtaa haina mishahara bali ina posho, kama umeamua kugombea maana yake unajua kuwa kwenye uenyekiti hakuna mshahara, usiende kutafuta msharaha kupitia kwa hawa wananchi na kuwasumbua, mihuri isiwe kitega uchumi, mkifanya hivyo tutagombana na sitaogopa kuwatetea wananchi,” amesema Gambo.

Aidha, Mbunge huyo amesema wenyeviti hao waende kuwatetea vijana, kina mama na wenye ulemavu kwenye mitaa yao ili wanufaike na mikopo inayotolewa na halmashauri ya jiji hilo kwani siasa za porojo zimeshapitwa na wakati.

Send this to a friend