Geita: Mama N’tilie adaiwa kuwalisha watu viungo vya binadamu

0
60

 

Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma imewapandisha kizimbani Mtoto mwenye umri wa miaka 15 (jina limehifadhiwa) pamoja na Juliet Makoye (43) wakazi wa Geita, wakidaiwa kuiba mtoto mwenye umri wa miaka 3 na miezi 6 katika Manispaa ya Musoma Mjini mkoani Mara.

Washitakiwa hao walifikishwa jana mahakamani hapo mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Stanley Mwakihaba na kusomewa maelezo ya awali na Wakili wa Serikali Monica Hokololo, akiieleza Mahakama kuwa mtoto huyo na Juliet walitenda kosa hilo Februari 10 mwaka huu katika mtaa wa Nyakato Mlimani.

Awali Wakili Hokololo ameieleza mahakama kuwa mtoto huyo ambaye ni mshitakiwa wa kwanza, alisema siku ya tukio alifika Mtaa wa Nyakato akitokea mkoani Geita kwa lengo la kuiba mtoto. Ilidaiwa kuwa mshitakiwa alimkuta mtoto huyo (aliyeibwa) amekaa nje peke yake, akamuita na kumbeba kisha akaondoka naye.

Inadaiwa kuwa walipofika mbali kidogo alimlisha dagaa zilizokuwa na dawa ya kumfanya apoteze uwezo wa kuzungumza, kisha akamfumua rasta aliizokuwa amesukwa, akamsuka mabutu na kumbadilisha nguo zake. Kwa Mujibu wa Hokololo amedai kuwa shida ilianzia kwenye kuita ungo (usafiri wa kichawi) ili uwapeleke mkoani Geita, kwani licha ya kufanya mazingaombwe yote juhudi hazikufanya kazi.

Wakili anaeleza kuwa mshitakiwa aliendelea kuranda mitaani mpaka alipokutana na dereva wa bodaboda aliyemhoji sababu za kuwa mtaani na mtoto usiku. Mtoto huyo alidai kuwa wametoka Geita na walikuwa wakimtafuta mama yao na hawakuwa wakijua jinsi ya kumpata, hivyo dereva huyo aliwapeleka kwa Mtendaji Mtaa wa Kigera, baada ya Mtendaji kupata mashaka juu ya maelezo yake akawapeleka kituo cha kati cha Polisi.

Kupitia maelezo ya Hokololo kesho yake wazazi wa mtoto aliyepotea walipeleka polisi taarifa za kupotelewa mtoto, na walipokutanishwa na Watoto hao ilibainika mshtakiwa hakuwa dada wa mtoto aliyeibwa.

Maelezo ya mshitakiwa yanadai kuwa amekuwa akitumwa na Juliet kuiba watoto, na kama angefanikiwa kumpeleka mtoto huyo  idadi ya Watoto ingefika watano. Amedai kuwa watoto anaowaiba ni umri kati ya miaka miwili hadi mitano wa jinsia yoyote, na huchinjwa anapowafikisha kwa Juliet, kisha viungo vyao vinauzwa kwa baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini katika migodi na nyama nyingine huzichoma na kuzila, kisha baadhi  huziuza kama kitoweo mgahawani.

Polisi walifanikiwa kumkamata Juliet akiwa kwenye biashara yake ya Mgahawa kama  ilivyoelezwa awali na mtoto huyo, washitakiwa wote wawili wamerudishwa rumande hadi Machi 28 mwaka huu ambapo kesi hiyo itasikilizwa tena.

Chanzo: Habari Leo

Send this to a friend