Na. Costantine James, Geita.
Wachimbaji wadogo wa madini mkoani Geita wametakiwa kuachana na imani potofu ya kwenda kwa waganga wa jadi kuchinja kuku katika maduara kwa lengo la kubaini madini yalipo, badala yake watumie teknolojia ya kisasa kwa kupeleka sampuli maabara za kisasa ili kubaini uwepo wa madini katika sehemu husika.
Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) mkoa wa Geita, John Kalimenze amesema kuna baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini wanatumia wanganga wa jadi katika shughuli za uchimbaji wa madini kwa lengo la kubaini madini yalipo.
Amesema imani za kishirikina zina athari kubwa kwa wachimbaji wadogo kwani mara nyingi wamekuwa wakipoteza pesa pamoja na muda kwa kuchimba madini katika sehemu ambayo hayapo.
Nao baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini waliojitokeza katika maonesho ya tano ya kitaifa ya teknolojia ya madini yanayofanyika katika viwanja vya Bombambili mkoani Geita wamekiri kufanya hivyo kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kutambua sehemu madini yalipo.