Gharama ya kufunga mfumo wa gesi kwenye magari yafikia milioni 2

0
58

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imebaini kuwa gharama kubwa za ufungaji wa mfumo wa gesi kwenye magari nchini zimechangia uwepo wa idadi ndogo ya magari yaliyofungwa mfumo huo.

Taarifa hiyo imesomwa leo bungeni Dodoma na mwenyekiti wa kamati hiyo, David Mathayo ambapo imebainisha kuwa wastani wa kufunga mfumo wa gesi kwa kila gari ni shilingi milioni 2, gharama ambazo sio kila Mtanzania anaweza kuzimudu.

Aidha, kamati imeeleza kuwa sababu nyingine ni uchache wa vituo vya kujazia gesi, pamoja na uchache wa watalaamu hususani wakaguzi wa mifumo hiyo ambao idadi ya waliosajiliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ni 10 pekee.

Biteko: Upungufu wa umeme umepungua baada ya mvua kunyesha

“Hadi kufikia Januari, 2024 kulikuwa na jumla ya vituo vitano kwa ajili ya kujaza gesi asilia kwenye magari ambapo kati ya vituo hivyo, vitatu vimejengwa Dar es Salaam, kimoja Pwani na kimoja Mtwara ambacho kinahudumia magari ya kampuni ya saruji ya Dangote,” imeeleza taarifa.

Kamati hiyo imesema kuna haja kwa Serikali kuongeza jitihada za kujenga vituo vya kutosha na kuongeza mtandao wa gesi nchini hususani maeneo ya kimkakati vikiwemo vituo vya GPSA, ili kuwezesha upatikanaji wa gesi hiyo kwa wingi na kwa urahisi.

Send this to a friend