Gharama za kuingia Kenya zapanda baada ya Serikali kuondoa visa

0
41

Baada ya uamuzi wa Serikali ya Kenya kutangaza kuondoa visa kwa wageni wote kutoka barani Afrika, baadhi ya wageni wamelalamikia utaratibu huo mpya kuwa ni mgumu na wenye gharama ukilinganishwa na hapo awali.

Mamlaka ya Kenya imefafanua kwamba ingawa nchi hiyo inatoa visa bila malipo, wageni wanahitaji kuwasilisha maombi ya idhini ya usafiri ya kielektroniki (ETA) kwa kutoa nyaraka zinazohitajika na kulipa ada ya dola 30 (TZS 75,540).

Kwa mujibu wa taarifa, sharti hilo pia linatumika kwa nchi ambazo raia wake walikuwa na idhini ya kuingia nchini Kenya bila kuhitaji visa.

Mwandishi maarufu kutoka Zimbabwe, Hopewell Chin’ono, katika ukurasa wake wa X aliandika kuwa “Ndugu Waafrika, Kenya haijaambia ulimwengu ukweli inaposema kwamba sasa haina visa, sivyo! Imefanya usafiri kuwa ngumu zaidi kwa Waafrika ambao hawakuhitaji visa hapo awali.”

Kulingana na mamlaka ya Kenya, nchi hiyo imepokea zaidi ya maombi 9,000 ya visa kupitia mfumo wa kidijitali huku wananchi wakielezea wasiwasi wao kwamba vikwazo hivyo vinaweza kusababisha baadhi ya wageni kususia nchi hiyo.

Chanzo: BBC Swahili

Send this to a friend