Google yashtakiwa kwa kuiba taarifa za watumia kivinjari binafsi

0
13

Kampuni ya Google imeburuzwa mahakamani nchini Marekani kwa tuhuma za kuingilia usiri wa mamilioni ya watu kwa kukusanya taarifa za matumizi yao ya intaneti hata wanapotumia kivinjari (browser) binafsi.

Katika kesi ya msingi Chasom Brown, Maria Nguyen na William Byatt wameiomba mahakama kuiamuru Google kulipa $5 bilioni (TZS 11.6 trilioni) kutokana na kukusanya taarifa za watu ikiwa ni pamoja na nini wanaangalia mtandaoni na wanajivinjari (browse) wapi licha ya kutuhumia huduma ya Incognito Mode, ambayo inaizuia Google kukusanya taarifa zao.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizowasilishwa mahakamani huko San Jose, California, Google inatuhumiwa kukusanya taarifa kwa kutumia huduma zake kama Google Analytics, Google Ad Manager, na programu tumishi nyingine na ‘plugins’ kwenye tovuti.

Taarifa hizo zinaisadia Google kufahamu marafiki wa mtumiaji, anapendelea nini, chakula chake bora, ununuzi wake wa bidhaa, masuala yake ya mahusiano ya kimapenzi na hata mambo mengine ya kutia aibu ambayo watumiaji wa intaneti hutafuta mitandaoni.

Upande wa mashtaka umesema watu walioathirika na njama hizo ni mamilioni ya waliokuwa wakitumia huduma hiyo binafsi (incognito mode) tangu ilipozinduliwa Juni 1, 2016.

Msemaji wa Google, Jose Castaneda amesema kampuni hiyo itajitetea yenyewe dhidi ya madai hayo.

Send this to a friend