Kampuni ya GSM imetangaza rasmi kujitoa katika udhamini mwenza wa ligi kuu soka Tanzania bara baada ya mkataba wao kwenda vibaya.
Pia wametangaza kuwa Ghalib Salim Mohamed maarufu kama GSM ameamua kujiuzulu katika nafasi yake ya Uenyekiti na Ujumbe wa kamati ya ushindi ya Taifa Stars.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya GSM yaliyopo Posta, Ofisa Biashara wa GSM, Allan Chonjo amesema kuwa waliwaandikia barua TFF baada ya kuona mabadiliko na ilivyo kwenye mkataba
“Haya hayajawa maamuzi rahisi kwa kampuni ya GSM kwani tunatambua vipo baadhi ya vilabu vya mpira pamoja na wadau mbalimbali wataumizwa na hatua hii, haikuwa dhamira yetu kufikia uamuzi huu mgumu,” amesema Chonjo.
Ameongeza “Upande wa klabu udhamini wa klabu tutaendelea kuwa kwenye mkataba wetu kama kawaida bali tumejitoa upande huu wa Ligi.”
Kampuni ya GSM iliingia Mkataba na ligi kuu wenye thamani ya shilingi Bilioni 2.1 kama mdhamini mwenza kwa kipindi cha miaka miwili.
Mkataba huo wa TFF na GSM umedumu kwa muda wa siku 76 tangu uliposainiwa Novemba mwaka jana