Halima Mdee agoma kuzungumzia walivyofika bungeni
Mwanasiasa Halima Mdee amesema hawezi kuzungumzia mchakato uliowafikisha bungeni hadi kuapishwa kwa sababu maelezo hayo yapo kwenye rufaa yao ya kupinga kuvuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mdee amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mvutano unaoendelea ndani ya chama hicho akiwa ameambatana na wenzake 18 ambapo wameapishwa kuwa Wabunge wa Viti Maalum.
“… vitu vyote vinavyohuskana na michakato hii, vipo kwenye mfumo wetu wa rufaa sitazungumza hapa. Ikifika wakati itazungumzwa,” amesema mwanasiasa huyo aliyekuwa Mbunge wa Kawe wakati akizungumza kwa niaba ya wenzake.
Mvutano huo umetokana na wanasiasa hao kuapishwa kushika nyadhifa hizo kupitia CHADEMA, huku chama chenyewe kikisisitiza kuwa hakijafanya uteuzi wa wabunge wa viti maalum.
Kutokana na hatua hiyo ambayo chama kimetafsiri kuwa ni ukiukwaji wa katiba, Kamati Kuu ya CHADEMA ilifikia uamuzi wa kuwavua uanachama na nafasi zao za uongozi wale wote walioapishwa bungeni.
Licha ya kukata rufaa, wanasiasa hao wamesema kuwa wataendelea kuwa wanachama wa hiari wa CHADEMA kwani wanakiheshimu chama hicho na wataendelea kufuata taratibu zote.
Kuhusu hatima ya rufaa yao wamesema wasiporidhika na uamuzi wa Baraza Kuu la CHADEMA watakwenda mahakamani.