Halmashauri ya Jiji la Arusha yafunga maduka ya wanaodaiwa kodi

0
54

Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo ameeleza kushangazwa na kitendo cha Halmashauri ya Jiji la Arusha kuendelea kufunga maduka ya wafanyabiashara wanaodaiwa kodi katika maeneo ya Stendi Ndogo na Soko la Kilombero, angali walikubaliana yafunguliwe.

Akizungumza na waandishi wa habari Gambo amesema kuwa akiwa na wafanyabiashara walikutana na uongozi wa halmashauri na kulizungumzia hilo ambapo walikubaliana maduka hayo yafunguliwe ili wafanyabiashara waendelee kuuza wapate fedha za kulipa kodi.

“… toka tumemaliza kikao kile zimepita zaidi ya siku tano sasa maduka bado hayajafunguliwa. Kipindi hiki cha sikukuu ndicho kipindi ambacho wafanyabiashara wengi wanafanya biashara nyingi sana,” amesema Gambo.

Mbunge huyo ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema kuwa serikali ilishazuia halmashauri na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufunga biashara za wanaodaiwa kodi, badala yake wakae chini na kuangalia namna kodi inaweza kulipwa na biashara ziendelee.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo, Abdi Mchomvu amesema jumla maduka 15 yamefungwa sokoni hapo na kwamba itakuwa vigumu kwa wafanyabiashara hao kulipa madeni yao wakati hawafanyi biashara.

Send this to a friend