Hashim Rungwe asema ukata unakwamisha kampeni za vyama vya siasa

0
70

Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimesema kuwa vyama vya siasa vinakabiliwa na ukata, hali inayopelekea vyama hivyo kushindwa kufanya kampeni kama ambavyo ratiba inaonesha.

Hayo yamesema na mgombea Urais wa Tanzania kupitia chama hicho, Hashim Rungwe ambaye amejizolea umaarufu miongoni mwa Watanzania kutokana na kaulimbiu ya chama chake ya kuhakikisha watu wanakula ubwabwa endapo atachaguliwa.

Rungwe ameeleza kuwa vyama vimeomba NEC kufanya mabadiliko ya ratiba ya kampeni zao kuelekea Oktoba 28, na kwamba yeye ataendelea na kampeni mara tu ratiba mpya itakapotolewa.

“Hatupewi ruzuku kutoka serikalini na hiyo ndiyo sababu tunashindwa kufuata namna ratiba inavyoonesha,” amesema Rungwe akifanya mahojiano na Mwananchi Communication Limited.

CHAUMMA kilizindua kampeni zake Septemba 5 jijini Dar es Salaam na kwa muda wote hakijatoka nje ya mkoa huo. Hata hivyo Rungwe amebainisha kuwa akianza tena kampeni ataanzia Kibaha mkoani Pwani.

Mbali na kuahidi ubwabwa mashuleni amesema chama chake kitavutia wawekezaji kwa kuweka mazingira rafiki lakini pia kilimo, ufugaji, viwanda, miundombinu vitapewa kipaumbele kwenye serikali yake.

Kufanikisha haya amesema serikali itapunguza matumizi ikiwa ni pamoja na kuacha kutumia magari yanayotumia mafuta mengi.

Amesisitiza kuwa ili watu waweze kuendelea, ni lazima kwanza wale vizuri.

Send this to a friend