Jamii ina mazoea ya kuwakanda kwa maji moto wanaojifungua kutokana na utamaduni wao unaobeba imani kwamba kwa kufaya hivyo kunarejesha maumbile ya mwanamke (tumbo na sehemu za siri) aliyokuwa nayo kabla ya kujifungua.
Hakuna uthibitisho wa kitaalamu kwamba jambo hilo linasaidia badala yake wataalam wa afya wanasema kwa kufanya hivyo husababisha madhara makubwa ikiwemo kutokwa na damu nyingi na hata vifo.
Madhara yanayotajwa ni pamoja na kumsababishia mhusika maumivu makali, kuharibu maumbile yake, kulegeza misuli, majeraha yanayosababishwa na maji ya moto, kuzuia uponyaji wa haraka, kusababisha maambukizi na tatizo la kisaikolojia kwa hofu ya kukandwa.
Akizungumza kwa kina, mtaalamu Agness Ndunguru amesema wamekuwa wakipokea visa vingi vinavyotokana na mwanamke aliyejifungua kukandwa maji moto ikiwemo mshono kufumuka na madhara mengi mengi.
“Hakuna uchafu unaotakiwa kutolewa na maji ya moto kwa kukandwa au kuminywa tumboni. Njia hii haina msaada hata kidogo, zaidi ni kupoteza muda tu kumminya mama nyumbani,” amesema.
Kenya: Wanawake wanawalipa wanaume milioni 5 wawape mimba
Ameongeza “Mara zote jamii hudhani damu zinazotoka baada ya kumkanda mama ni uchafu uliobaki baada ya kujifungua. Ni makosa makubwa, kwani maji moto hufungua mishipa ya damu iliyojifunga baada ya mtoto kutoka na damu huanza kuvuja upya,”
Aidha, ameshauri kuwa wanawake wanaweza kukanda viungo vyao ikiwemo mabega na miguu kwa maji ya vuguvugu na si ya moto na kwamba wanatakiwa wapate muda wa kutosha wa kupumzika pamoja na kufanya kazi ndogondogo za nyumbani, hiyo itamsaidia mwanamke kurudisha mwili katika maumbile yake ya asili.
Mbali na hayo, amesema ulaji wa mtori kwa wingi wakati wa kujifungua si mlo kamili wa kumfanya mama kurudisha mwili, bali mlo kamili ikiwemo ugali laini, mboga za majani kwa wingi, maji na protini ndio vinaweza kumsaidia mama kupata maziwa ya kutosha na kurudisha mwili wake wa asili.
Chanzo: Habari Leo