Hati Fungani ya NMB Jamii Yaandika Historia kwa Kukusanya Tsh Bilioni 400

0
66

Historia imeandikwa katika Masoko ya Mitaji Afrika Mashariki, baada ya Hati Fungani ya NMB Jamii kukusanya Tsh Bilioni 400, ikiwa ni zaidi ya mara tatu ya lengo lililokusudiwa.

Hati Fungani hiyo imekusanya jumla ya Tsh Bilioni 212.9 kwa fungu la Shilingi za Kitanzania na Dola za Kimarekani Milioni 73 kwa fungu la Dola za Kimarekani.

Matokeo haya yametangazwa rasmi wakati wa hafla ya kuiorodhesha Hati Fungani ya NMB Jamii katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mapema leo.

Fedha zote zilizopatikana kupitia Hati Fungani ya Jamii, zitaelekezwa katika kutoa mikopo nafuu kwenye miradi endelevu, ikiwemo miradi ya nishati mbadala, miradi ya kuzuia na kudhibiti uchafuzi wa mazingira, miradi ya maji, miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, miradi ya wanawake, vijana, elimu, afya, nyumba nafuu na mingine inayoendana na hiyo.

NMB Jamii Bond ilizinduliwa na kuanza kuuzwa Septemba 25 hadi Oktoba 27 mwaka huu.

Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya Hati Fungani hiyo na kuiorodhesha DSE, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, amesema: “NMB Jamii Bond ilikuwa imegawanyika katika mafungu mawili, fungu la kwanza likihusisha Shilingi za Kitanzania na fungu la pili la Dola za Kimarekani, ambako kote tumevuka lengo la makusanyo, kwa upande wa Shilingi tukipata Bilioni 212.9 kutoka Bil. 100 za lengo na upande wa Dola tukikusanya Milioni 73 badala ya Milioni 15.

“Kwa mantiki hiyo, thamani ya jumla ya fedha zilizopatikana kutokana na NMB Jamii Bond ni Sh. Bilioni 400, ambazo ni mara tatu zaidi ya lengo tulilokuwa nalo” amebainisha Bi. Zaipuna huku akiwahakikishia wateja zaidi ya 5,600 walionunua Hati Fungani hizo kuwa pesa zao ziko mikono salama.

“Tunawashukuru wateja wetu na wawekezaji wote kwa kutuamini na kusimama pamoja nasi katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii,” amesema Bi. Zaipuna.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa hafla hiyo aliipongeza NMB kwa kuweka rekodi ya Bilioni 400 za mauzo ya Hati Fungani hiyo.

“Hati Fungani ni fursa muhimu kwa jamii kunufaika kwa njia mbili za kuweka akiba, lakini pia kufanya uwekezaji wenye faida kubwa. Bond ni mkopo ambao taasisi ya fedha inakopa kwa wananchi. NMB ingeweza kwenda kukopa BoT au benki za nje, lakini ikachagua kukopa kwa wananchi kupitia mdhamana wao ambaye ni CMSA na inarejesha kwa riba kubwa ya asilimia 9.5.

“Pongezi zangu kwa NMB pia kutokana na unyeti na umuhimu maeneo wanakozielekeza pesa hizi, kwa sababu mnaenda kuisaidia pakubwa sana Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, lakini pia nikiri kwamba Hati Fungani hii imeniheshimisha mno mimi kwa Rais, kwani imeingiza Dola za Marekani Milioni 73 katika kipindi hiki cha uhaba wa Dola nchini.

“Rekodi hii ya mauzo inaweza kuwa ya kushangaza kwa taasisi zingine, lakini kwa NMB hili sio la kushangaza kutokana na ufanisi wake, ikitajwa mara 10 na Majarida ya Euromoney, Global Magazine, African Bankers na mengine kuwa ni Benki Bora na Salama Zaidi Tanzania, huku Afisa Mtendaji Mkuu wake akitwaa tuzo kadhaa za CEO Bora wa Mwaka wa Afrika,” amesisitiza Prof. Kitila.

Zoezi hili limefanyika mbele ya Mgeni Rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji – Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB – Ruth Zaipuna, Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania – Mhe. David Concar, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) – CPA. Nicodemus Mkama, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE – Mary Mniwasa, pamoja na wawakilishi kutoka International Finance Co-operation, Orbit Securities na taasisi zingine.

Send this to a friend