Hatma ya Ligi Kuu Tanzania Bara kujulikana kesho

0
52

Ikiwa ni takribani miezi miwili sasa tangu Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara iliposimamishwa kutokana na janga la corona, hatma ya mashindano hayo inatarajiwa kufahamika kesho Mei 3, 2020.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo amesema hatma hiyo itafahamika baada ya bodi ya ligi kukutana, kwani kikao hicho ndicho kitakachoamua kama msimu huu wa mwaka 2019/2020 utaendelea, au ndio umefikia tamani.

“Katika hiki kikao kutakuwa na muelekeo sasa wa ligi yetu kwa msimu wa 2019/20 kwamba unaelekea wapi,” amesema Kasongo.

Kasongo ameongeza kuwa uamuzi utakaofikiwa kesho, kabla ya kuanza kutekelezwa utapelekwa kwenye baraza ambalo linahusisha vilabu vyote ambalo linatoa uamuzi wa mwisho, kisha utapelekwa kwenye kamati ya utendaji.

Wachambuzi wa soka wameeleza kuwa maamuzi matatu yanaweza kufikiwa ikiwa ni Simba SC inayoongoza ligi kupewa ubingwa, ligi iendelee hali itakapokuwa shwari au msimu ufutwe kama ilivyofanya Uholanzi.

Wakati hayo yakitokea Tanzania, nchini Kenya klabu ya Gor Mahia ametawazwa kuwa mabingwa, huku PSG ya Ufaransa nayo ikikabidhiwa kombe licha ya ligi hizo kutomalizika.

Send this to a friend