Hatua za kisheria za kuchukua mchumba anapovunja ahadi ya kuoana

0
61

Haitakua haki kama kutakua na mfumo au namna inayolazimisha watu kuoana kama watu hao hawataweza kuishi pamoja kwa furaha. Suala la ndoa ni muunganiko unaohitaji ridhaa ya mwanaume na mwanamke (au wanawake kama ndoa ni ya mke zaidi ya mmoja).

Lord Kenyon katika kesi ya Atchinson v. Baker alisema, “….it would be most mischievous to compel parties marry who could never live happily together.” Maneno haya yanadhihirisha kua hakuna sheria au mamlaka yoyote inayoweza kulazimisha watu kuoana, isipokua kwa ridhaa yao na pia kuzingatia misingi na vigezo vingine vilivyowekwa na kutambuliwa kisheria.

Kimsingi, andiko hili linalenga kukupa mwanga juu ya namna gani suala la kuvunja ahadi ya ndoa (breach of promise to marry) linatambulika na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hasa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 na kueleza kwa kifupi haki za wahusika katika uchumba huo pindi ahadi kuoana inapovunjika.

Sababu za msingi zinazoweza kepelekea uchumba kuvunjika; Kuna sababu mbalimbali ambazo zinaweza kupelekea uchumba kuvunjika hivyo lengo la kufunga ndoa kutofikiwa baina ya wachumba hao.

Sababu hizo nitazieleza katika makundi matatu kama ifuatavyo;

Kwanza, kutokuweka bayana masuala ya msingi kwa mchumba wako, hasa masuala yale ambayo kimsingi unatakiwa kuyaweka wazi. Mfano; utofauti wa dini na taifa, ugonjwa wa ulevi (dipsomania), utasa au ugumba (sterility) na kadhalika.

Pili, kuvunja makubaliano. Mfano, kama mmoja kati ya wachumba hao anafanya matendo kinyume na maadili na mtu wa tatu (kama kuchepuka – neno lisilo rasmi) au mmoja kati ya wachumba hao anakataa pendekezo la kufunga ndoa kwa muda mrefu pasipo sababu za msingi.

Tatu, mabadiliko makubwa kutokea kati ya wachumba baada ya kuingia katika uchumba huo ambayo yanahatarisha kufanikisha kufungwa kwa ndoa rasmi. Mfano; uhanithi (impotence), wazimu/ukichaa (insanity) baina ya wachumba na kadhalika.

Mali za wachumba; Ni suala la kawaida kwa wachumba kumiliki mali. Inawezekana kabisa katika engagement wachumba wakabarikiwa kuchuma mali. Swali linakuja je, mali hizo itakuaje pindi wachumba hao watakaposhindwa kufikia lengo lao au adhma ya kufunga ndoa kutokana na sababu moja au nyingine?

Kwa ufupi, kwakua uchumba sio ndoa kisheria, hivyo mali za wachumba hao haziwezi kuhesabika kama mali za familia (matrimonial assets). Hivyo basi zitakua ni milki ya mhusika katika uchumba huo, yaani kama mali ilikua ni ya mwanamume basi itakua ni mali yake mwenyewe, vivyo hivyo kwa mwanamke.

Ila, kama kati ya wachumba hao, mmoja wao akaamua kwa ridhaa yake kutoa mali yake kama zawadi kwa mchumba wake, basi mali hiyo itahesabika kua ni mali ya mchumba aliyepewa mali hio isipokua kama mtoaji anaweza kuthibitisha tofauti.

Zawadi za wachumba; Suala jingine la msingi kuzingatia ni zawadi baina ya wachumbaKatika jambo hili, swali la msingi kabisa kujiuliza ni je, zawadi hio ilitolewa na mchumba kwa mwenzake kama rafiki wa kawaida tu au kwa matarajio ya kuja kuwa mke/mume hapo baadae? Kama zawadi hio ilitolewa kwa lengo la pili, yaani kwa matarajio ya kuwa mume na mke hapo baadae, basi zawadi hio itakua yenye sharti yaani“conditional”. Ila kama zawadi hio ilitolewa na mmoja kati ya wachumba hao kama mtu wa kawaida tu, pasipo sharti, basi zawadi hio itakua ni mali binafsi ya mchumba huyo aliyepewa zawadi hio na inaweza kurudishwa.

Kifungu cha 71 cha sheria ya ndoa ya mwaka 1971, kinatoa haki ya kurudishiwa zawadi zilizotolewa na mmoja kati ya wachumba hao kwa matarajio ya kufunga ndoa lakini kwa sababu moja au nyingine ndoa hiyo haikufungwa. Hivyo mtoa zawadi ana haki ya kufungua shauri mahakamani kudai zawadi alizompa mchumba wake arudishiwe kwa kuithibitishia mahakama kua zawadi hizo alitoa kwa sharti la kufunga ndoa (that the gift(s) was conditional on the marriage being contracted) na sio vinginevyo. Mahakama lazima ijiridhishe kwamba zawadi hizo zilitolewa kwa sharti kwamba wachumba hao wana nia ya kufunga ndoa.

Haki ya kudai fidia kwa kuvunjwa ahadi ya kuoa/kuolewa (ndoa (Right to damages for breach of promise of marriage):

Kifungu cha 69 cha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kinatoa haki kwa wapenzi kupeleka shauri mahakamani na kudai fidia kutokana na kuvunjwa ahadi ya ndoa. Suala la msingi kuzingatia ni kwamba, hakuna shauri litakalokubalika kisheria kama mdaiwa katika shauri hilo wakati wa ahadi alikua na umri chini ya miaka kumi na nane. Pia, fidia haziwezi kutolewa zaidi ya hasara ambayo ndio dhahiri kwa upande wa mdai ambayo ilitokana na gharama alizoingia wakati wa ahadi hiyo na mambo mengine kama hayo.

Je, ni muda gani umewekwa kisheria kwa ajili ya kufungua madai ya fidia kutokana na kuvunjwa kwa ahadi ya kuoa/kuolewa (ndoa)?Kifungu cha 70 cha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kinaweka ukomo wa muda wa kupeleka shauri mahakamani kudai fidia za uvunjifu wa ahadi ya ndoa kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu ahadi hiyo ilipovunjwa.

Mwisho;Kwa kuhitimisha, sheria inatambua hatua mbalimbali ambazo mwanaume na mwanamke wanapitia kabla ya kufunga ndoa, ikiwa ni pamoja na uchumba na kadhalika. Hivyo, sheria imeweka namna ambayo mambo mbalimbali mfano mali na watoto wanaoweza kupatikana kabla ya ndoa rasmi kufungwa yanaweza kushughulikiwa endapo ndoa haitafungwa kabisa kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuvunja ahadi ya ndoa kama ilivyoelezwa hapo juu.

Na Aloyce Makendi (Mwanasheria)

Send this to a friend