Hawa ni watu 5 matajiri zaidi barani Afrika

0
45

Bara la Afrika linasifika kwa kuwa na talanta ya wajasiriamali ambao wamepanda ngazi ya mafanikio na utajiri. Sasa, takwimu mpya za Forbes za mwaka 2023 zimeweka wazi orodha ya mabilionea wa Afrika ambao wanaongoza katika ulimwengu wa biashara na utajiri.

Hii ni orodha ya mabilionea watano barani Afrika kwa mwaka 2023;

1. Johann Rupert & Family – TZS trilioni 28.97
Johann Rupert (73) kutoka Cape Town, Afrika Kusini ni mwenyekiti wa kampuni ya Compagnie Financiere Richemont, anaongoza orodha ya Forbes 2023 na utajiri wa dola bilioni 11.8 [TZS trilioni 28.97].

Kampuni yake inamiliki bidhaa maarufu kama Cartier na Montblanc. Mafanikio yake yameenea kwa muda mrefu, na uwekezaji wake mbalimbali umesaidia kuongeza utajiri wake. Pia amejulikana kwa kuhimiza uhifadhi wa mazingira kwa kupinga mbinu za kuchimba gesi kwa kutumia teknolojia ya fracking nchini Afrika Kusini.

2. Aliko Dangote – TZS trilioni 25.04

Aliko Dangote (66) kutoka Lagos, Nigeria ni mfanyabiashara maarufu na mfadhili barani Afrika, anashikilia nafasi ya pili kwenye orodha ya Forbes na utajiri wa dola bilioni 10.2 [TZS trilioni 25.04].

Utajiri wake unategemea kampuni ya Dangote Cement, ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya kuzalisha saruji barani Afrika na inaendesha shughuli katika nchi kumi. Biashara zake zinajumuisha pia uzalishaji wa sukari na pia juhudi zake za kukuza miundombinu ya Nigeria zimempa heshima kubwa.

3. Nicky Oppenheimer & Familia – TZS trilioni 20.6
Nicky Oppenheimer (78) kutoka Afrika Kusini, ni mrithi wa utajiri wa almasi wa DeBeers, anaongoza nafasi ya tatu kwa utajiri wa dola bilioni 8.4 [TZS trilioni 20.6]. Mbali na biashara ya almasi, Oppenheimer pia amefahamika kwa uwekezaji wake katika sekta ya anga, kupitia kampuni yake ya Fireblade Aviation na juhudi zake za uhifadhi katika nchi mbalimbali za Kiafrika.

4. Nassef Sawiris – TZS trilioni 18.4
Nassef Sawiris (62) kutoka Cairo, Misri ambaye ni mtoto wa familia tajiri zaidi nchini humo, anashikilia nafasi ya nne kwenye orodha akiwa na utajiri wa dola bilioni 7.5 [TZS trilioni 18.4].
Moja ya wazalishaji wakubwa zaidi wa mbolea za nitrojeni duniani aliyejikita pia katika uwekezaji. Pia ameingia katika ulimwengu wa michezo kwa kununua sehemu ya klabu ya soka ya Aston Villa katika Ligi Kuu ya England.

5. Nathan Kirsh – TZS trilioni 15.7
Nathan “Natie” Kirsh, mwenye umri wa miaka 91, ni mjasiriamali maarufu kutoka Eswatini (Swaziland) na anashika nafasi ya tano kwa utajiri wa dola bilioni 6.4 [TZS trilioni 15.7]. Yeye ni mmiliki wa hisa katika kampuni ya Marekani inayoitwa Jetro Holdings, ambayo inamiliki maduka maarufu ya kusambaza vifaa na migahawa kama vile Jetro Cash and Carry na Restaurant Depot.

Send this to a friend