Baada ya Dkt. Wilbroad Slaa kuvuliwa hadhi ya Ubalozi Septemba 01, mwaka huu na Rais Samia Suluhu Hassan, wengi wamejiuliza juu ya vitu gani ambavyo Dkt. Slaa atavipoteza baada ya hadhi hiyo kuondolewa.
Swahili Times imezungumza na Mhadhiri kutoka Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam, Godwin Gonde ambaye amefafanua kuwa hadhi ya ubalozi ni ya kudumu kwa maana kuwa mtu anapoteuliwa na kupewa hadhi hiyo haiondolewi isipokuwa mamlaka iliyomteua itakapoona mtu huyo amefanya kosa au mwenendo wake hauendani na hadhi aliyopewa.
“Hadhi ya ubalozi maana yake ni kuwa wewe bado ni mtu wa Serikali hata kama huna majukumu ya kiserikali, unapofanya vitendo ambavyo vinaenda kinyume na serikali ambayo ndiyo imekupa hadhi hiyo, mamlaka iliyokuteua inayo mamlaka ya kutoa hadhi hiyo, na inapoitoa maana yake kuna upendeleo wa kibalozi utaondoka pia,” ameeleza.
Akifafanua juu ya upendeleo huo, amesema balozi aliyepangiwa kituo cha kazi maana yake anapewa kinga na upendeleo, lakini kwa balozi ambaye hajapangiwa kituo hapewi kinga ila anapata upendeleo mdogo unaojumuisha kumiliki hati ya kusafiria ya kidiplomasia, kutambuliwa na mataifa ya nje na kupewa huduma maalum na ya heshima kwenye vituo vya kusafiria (terminals).
“Pasi ile inawaelezea mataifa ya nje kuwa mtu huyu ni wakala wa serikali, mumhudumie kwa heshima, msimkague, msimpangishe foleni, msimdhalilishe, msimuweke ndani, msimhoji, ndiyo upendeleo unaoupata ukiwa na hati ya kusafiria ya kidiplomasia,” ameongeza.
Aidha, amesema “mamlaka inapoitoa hadhi hiyo maana yake kuna upendeleo utaukosa, ambapo hutoitwa tena balozi na maana yake ni kuwa utakuwa raia wa kawaida, hutakuwa na upendeleo katika taasisi za kiserikali, hutopata upendeleo utakaposafiri na mataifa ya nje hayatakutambua kama balozi,” ameeleza Gonde.
TPA yatangaza fursa ya uwekezaji Bandari ya Dar es Salaam
Aidha, amesema kuwa ili mtu ateuliwe kuwa balozi lazima Serikali ijiridhishe kama anaendana na hadhi hiyo kwakuwa atasimama kama kioo kuiwakilisha serikali, hivyo anapovuliwa ubalozi ni “aibu kwake na kwa Serikali” ikitafsirika kuwa haikujiridhisha vya kutosha juu ya mwenendo wa mtu huyo aliyeteuliwa.
Hata hivyo, Gonde amesema hadhi ya ubalozi inaweza kurudishwa baada ya mamlaka kujiridhisha kuwa mtu huyo anafaa tena kuwa balozi licha ya kwamba hakuna mtu aliyewahi kurudishiwa hadhi hiyo katika historia ya Tanzania.
Dkt. Slaa aliteuliwa kuwa balozi Novemba 23, 2017 na amehudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Sweden akihudumia pia Denmark, Finland, Norway, Iceland, Estonia, Latvia, Ukraine na Lithuania kuanzia mwaka 2017 hadi Septemba 2021.