Haya ni makundi matatu yatakayofanyiwa majaribio ya dawa za corona

0
43

Mganga Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Prof. Abel Makubi ameeleza kuwa dawa za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona zilizoingizwa nchini kutoka Madagascar na zilizotengenezwa nchini zitafanyiwa uchunguzi kwanza kabla ya kuanza kutumika.

Akizungumza katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Prof. Makubi amesema ifahamike dawa zilizoletwa kutoka nje na ile iliyoandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) si za kugawa kwa wananchi kwa sasa.

“Dawa hizi si ya kugawa kwa wananchi kwa sasa, tutafanya kwanza utafiti kujua kama ni salama, na kuangalia ubora wake katika kukabiliana na virusi vya corona. Wenzetu #Madagascar wamejiridhisha ndio maana wameanza kutumia,” amesema Makubi.

Akielezea namna uchunguzi huo utakavyofanyika, amesema kutakuwepo na makundi matatu ya wagonjwa watakaojitolea ambayo yatapewa dawa tofauti ili kuona zinavyoweza kuwasaidia.

“Kundi la kwanza ni la wale watakaoendelea kutumia dawa za sasa zinazoendelea kusaidia kufubaza kirusi, kundi la pili ni wale watakaotumia dawa hizi za Madagascar, na kundi la tatu ni wale watakaotumia dawa ya Madagascar kwa kuongezea na ile iliyotengenezwa na NIMR,” amesema Makubi.

Akizungumza katika halfla hiyo Waziri wa Mambo ya Nje, Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakidharau dawa za asili, bila ya kufahamu kwamba ndio dawa bora katika kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

Tanzania imepokea zawadi hiyo ya dawa kutoka Madagascar ikiwa ni siku chache tangu Rais Dkt. Magufuli alipoueleza umma kuwa ameandikiwa barua na Rais wa Madagascar kuhusu uwepo wa dawa hiyo.

Send this to a friend