Haya ni matokeo ya Iptisum, mwanafunzi aliyebadilishiwa namba ya mtihani

0
12

Mwanafunzi wa Shule ya Chalinze Modern Islamic Pre and Primary iliyopo mkoani Pwani, Iptisum Slim, aliyebadilishiwa namba ya mtihani wa darasa la saba amefaulu kwa wastani wa daraja la A.

Hiyo ni baada ya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kutangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba na Kaimu Katibu Mtendaji wa NECTA, Athumani Almasi na kuonesha kuwa Iptisum amefaulu kwa wastani wa A, kwa kupata alama A katika masomo manne na B katika masomo mawili.

Masomo aliyopata A ni Kiswahili, English, Maarifa na Sayansi huku aliyopata B ni Hisabati na Uraia.

Akizungu muda mfupi baada ya matokeo hayo kutangazwa Iptisum amesema siri ya yeye kufaulu ni kusoma kwa bidii huku akiwashukuru wote waliomsaidia kupaza sauti.

Tazama hapa matokeo ya darasa la saba 2022

Awali ilisambaa video katika mitandao ya kijamii ikimuonesha mwanafunzi huyo akiomba msaada kwa Serikali baada ya kubadilishiwa namba yake ya mtihani na kupewa namba ya mtu mwingine.

Kutokana na hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alitangaza kufanya uchunguzi na kuifungia shule hiyo iliyopo mkoani Pwani kuwa kituo cha mtihani kwa muda usiojulikana.

Chanzo: Mwananchi.

Send this to a friend