Serikali imesema uchambuzi uliofanywa umebaini kuwa mikoa iliyo hatarini zaidi kupata ugonjwa wa Ebola ni Kagera, Mwanza, Kigoma, Geita na Mara.
Aidha, Mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Kilimanjaro, Songwe, Mbeya na Dodoma ipo katika hatari kwa sababu ya uwepo wa viwanja vya ndege na vituo vikubwa vya mabasi ya kutoka nchi jirani.
Ummy: Serikali tumependekeza bima ya afya kuwa lazima
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 28, 2022 Jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa uwepo wa ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani unaiweka Tanzania katika hatari kubwa kutokana na mwingiliano mkubwa wa shughuli za kiuchumi na kijamii kupitia mipaka rasmi na isiyo rasmi.
“Hadi sasa hakuna mgonjwa wa Ebola nchini Tanzania. Hivyo yatupasa kila mmoja wetu kuchukua hatua na kuhakikisha ugonjwa huu hauingii nchini,” amesema.
Ameongeza kuwa hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa na Serikali ili kuzuia ugonjwa kuingia nchini ikiwemo kuimarisha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo.