Seif Sharif Hamad alizaliwa Oktoba 22, 1943 huko Kisiwani Pemba.
Alipata elimu ya msingi kuanzia 1950 hadi 1957 katika shule za Uondwe na Wete kisiwani humo. Alianza elimu ya sekondari mwaka 1958 na kuhitimu 1961 kutoka King George VI Memorial Secondary School, Zanzibar
Baada ya Hapo alikwenda Same mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya elimu ya kidato cha tano na sita kuanzia mwaka 1962 hadi 1963.
Kwa miaka tisa baada ya hapoa (1964 hadi 1972) aliajiriwa kama mwalimu wa sekondari ikiwa ni mkakati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukabiliana na upungufu wa watumishi uliosababishwa na kuondoka kwa maafisa wa Kiingereza.
Alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1972 na alihitimu Shahada ya Awali ya Sanaa katika Sayansi ya Siasa, Uongozi wa Umma na Uhusiano wa Kimataifa (B.A. Political Science, Public Administration and International Relations) mwaka 1975.
Amewahi kuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri wa Elimu kuanzia 1977 hadi 1980, mjumbe mwanzilishi wa Baraza la Wawakilishi kuanzia 1980 hadi 1989, Mbunge wa Bunge la Tanzania (1977), Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM (1977-1987).
Baada ya mvutano ndani ya CCM alivuliwa uanachama wa chama hicho mwaka 1988 na kupoteza nafasi za uongozi alizokuwa nazo.
Tanzania ilipoanzisha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, yeye na waliokuwa wanachama wa CCM walianzisha Chama cha Wananchi (CUF), na katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi alikuwa mgombea wa Urais Zanzibar kupitia CUF na kupata kura 49.76%.
Baada ya hapo amegombea chaguzi sita na mara zote ameshindwa na mgombea wa chama tawala ambapo katika uchaguzi wa mwaka 2020, aligombea kupitia ACT-Wazalendo.
Machi 2019 alijiuzulu kutoka CUF (akiwa Katibu Mkuu) na kujiunga ACT-Wazalendo, ambapo alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho.
Disemba 2020 Maalim Seif aliapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar baada ya kushika nafasi ya pili katika uchaguzi wa mwaka huo.
Januari 31, 2021 chama chake kilitangaza kuwa alikutwa na maambukizi ya virusi vya Corona na kwamba afya yake ilikuwa ikiimarika baada ya matibabu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi ametangaza kuwa Seif Sharif Hamad amefariki dunia leo Februari 17, 2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.