Historia: Homa kali ya mafua ilivyoiathiri Afrika Mashariki mwaka 1918
Wakati duniani ikiendelea kukabiliana na janga la mlipuko wa homa ya mapafu (COVID-19) inayosababishwa na virusi vya corona, historia inaonesha kuwa virusi hivi si janga la kwanza kuwahi kuitikisa dunia.
Mwaka 1918 hadi 1919 dunia ilikumbwa na mlipuko wa Spanish flu ambapo kwa mujibu wa makala iliyoandikwa na David Killingray (https://t.co/idVcvlmGMl), ugonjwa huo ulisambaa kwa kasi katika maeneo mbalimbali, huku maeneo machache sana yakinusurika.
Wimbi la kwanza la ugonjwa huu lilianza Machi 1918 nchini Marekani na kusambaa kwa haraka barani Ulaya, Asia, Australia na Kaskazini mwa Afrika. Wimbi la pili lililopelekea vifo zaidi lilianza Agosti 1918, ambapo taarifa zinaeleza kuwa lilianzia Ufaransa na kisha kuitafuna dunia nzima.
Inakadiriwa kuwa Spanish flu ili sababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 30 duniani kote, idadi kubwa zaidi kuliko ya waliofariki katika Vita vya Kwanza vya Dunia (WW1). Ugonjwa huu ulikuwa ni hatari zaidi kuwahi kuikumba dunia tangu maradhi ya ‘Black Death’ yalipotokea katika Karne ya 14.
Kama ilivyo kwa virusi vya corona, Spanish flu ilikuwa ikiathiri mfumo wa upumuaji, ilianzia sehemu moja, ilichukua muda mfupi tangu mtu alipoambukizwa hadi dalili kuonekana, na ilisambaa zaidi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu.
Miongoni mwa dalili zake ilikuwa ni pamoja na kukohoa damu na kutoka damu puani. Idadi kubwa ya vifo ilitokana na mapafu kushindwa kufanya kazi.
Athari zake Afrika Mashariki
Kwa kiasi fulani imekuwa ni vigumu kubaini madhara yaliyosababishwa na ugonjwa huu katika nchi za Afrika Mashariki kwa sababu wakati mlipuko huo ukiendelea, ukanda huu ulikuwa ukikabiliwa na matatizo mengine ambayo ni vita, njaa, ukame, na magonjwa mengine kama ndui (smallpox) na ‘rinderpest.’
Wimbi la pili la Spanish flu liliingia Afrika Mashariki kupitia meli iliyotoka Bombay nchini India Septemba 1918, na uliingia ndani ya nchi na kuathiri maeneo yaliyomo pembezoni mwa reli.
Ndani ya siku chache Nairobi iliathiriwa na kuanzia kipindi hicho hadi kufikia mwisho wa mwaka takribani nchi yote (Kenya) ilikuwa imeathiriwa, hasa kutokana na shughuli za kivita. Ilipofika Oktoba, ugonjwa huo ulikuwa tayari umezishambulia Uganda na Tanganyika (Tanzania Bara). Mamlaka visiwani Zanzibar ziliweza kuvilinda visiwa hivyo kwa kuwa na sheria kali za karantini.
Katika maeneo ya Kusini mwa Tanganyika karibu kila nyumba ilikuwa na muathirika na katika Wilaya ya Tukuyu moja ya kumi ya idadi ya watu wote, 180,000 wanaripotiwa kuwa huenda walifariki dunia. Idadi ya watu waliofariki nchini kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo inakadiriwa kuwa zaidi ya 100,000.
Nchini Kenya, takribani watu 150,000 ambao walikuwa sawa na asilimia 5.5 ya watu wote walifariki dunia, huku Uganda ikiwa na idadi ndogo zaidi ya vifo.
Ugonjwa huu ulilipuka kwa haraka na kupelekea vifo vya watu wengi, kwani mataifa mbalimbali hayakuwa yamejiandaa lakini pia uwezo wa kukabiliana nao ulikuwa mdogo.
Licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko hasa virusi tangu mwaka 1919, magonjwa hayo bado yameendelea kuwa changamoto huku yakigharimu maisha ya watu wengi.
Pamoja na mambo mengine, Spanish flu ilibadili mifumo ya maisha ya watu hata baada ya kutokomezwa, jambo ambalo baadhi ya wanasayansi wameeleza kuwa litatokea pindi dunia itakatokomeza virusi vya corona. Wanasayansi hao wamesema kuwa mfumo wa maisha hautorudi kuwa kama ulivyokuwa awali, bali binadamu watakuwa na taratibu nyingine za kimaisha, kutokana na athari za ugonjwa wa corona.