Historia: Simulizi fupi ya Brigedia Nyirenda walivyopandisha Mwenge wa Uhuru Mlima Kilimanjaro 1961

0
132

Mwaka 2021 Kilele cha Mbio za Mwenge Kitaifa kinafanyika mkoani Geita ambapo kinakwenda sambamba na maadhimisho ya Mika 22 ya kifo cha Mwl. Julius Nyerere.

Mwalimu Nyerere ndiye mwasisi wa Mwenge wa Uhuru na alipouwasha alisema, “Tunawasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike hata nje ya mipaka ya nchi yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa dhaarau.”

Je! Una mfahamu aliyeupandisha mwenge huo juu ya Mlima Kilimanjaro ili kutimiza malengo hayoyaliyosemwa na Hayati Mwl. Nyerere?

Brigedia (Mtf) Alexander Gwebe-Nyirenda alizaliwa Februari 2, 1936 Karonga Malawi, wakati wazazi wake wakiwa katika likizo ndefu ya Krismasi kutoka Tanganyika.

 

Alisoma shule ya msingi ya Mchikichini Dar- Es-Salaam na baadaye shule za Sekondari za Wanaume za Malangali (mkoani Iringa) na Tabora, hadi 1957.

Alex Gwebe-Nyirenda Jnr. akiwa na picha ya marehemu babu yake kwenye Makaburi ya Kinondoni ambako shujaa huyo aliyepandisha Mwenge wa Uhuru kilele cha Mlima Kilimanjaro alipozikwa (Desemba 24, 2008).

Alex Gwebe-Nyirenda Jnr. akiwa na picha ya marehemu babu yake kwenye Makaburi ya Kinondoni ambako shujaa huyo aliyepandisha Mwenge wa Uhuru kilele cha Mlima Kilimanjaro alipozikwa (Desemba 24, 2008).

Baada ya kuchaguliwa kuendelea na amali ya kijeshi, alijiunga na Chuo cha Kifalme cha Kijeshi cha Sandhurst kama Afisa Kadeti mwaka 1958 na baada ya kufuzu alirejea Tanganyika kujiunga na King’s African Rifles mwaka 1960.

Alipandishwa cheo kuwa Afisa Kamili katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na aliondoka jeshini kama Luteni-Kanali Agosti 1964.

Ilikuwa Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi aliyempa heshima kwa kumpandisha cheo cha Brigedia pamoja na marehemu Brigedia Mstaafu, Moses Nnauye.

Alikuwa Mtanganyika wa kwanza kuhitimu kutoka Chuo cha Kifalme cha Kijeshi cha Sandhurst, akiwa katika kombania ya Waterloo. Alikuwa afisa wa kwanza Mtanganyika katika King’s African Rifles 1960.

Alipewa heshima ya kupandisha Bendera ya Tanganyika kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro Desemba 9, 1961, ambapo wakati huo huo bendera hiyo ilikuwa ikipandishwa Uwanja wa Taifa katika mji mkuu wa taifa jipya la Tanganyika, Dar-es-Salaam.

Nyirenda alifanya kazi hiyo kwa ujasiri mkubwa, ikikumbukwa kuwa wakati huo, kupanda mlima huo mrefu zaidi barani Afrika ilikuwa ni jambo kubwa, zito na la hatari kutokana na ukweli kwamba kulikuwa na barafu nyingi, teknolojia ilikuwa ndogo na watu wengi waliogopa wakiamini kuwa uwezekano wa kurudi chini ukiwa hai ulikuwa mdogo.

Nyirenda alisema msafara wa kupanda Mlima Kilimanjaro ulikuwa na watu 11, wakiwemo wapiga picha na watangazaji wa redio. Safari yao ilianza jijini Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro ambapo walitumia jumla ya siku 16 kutimiza wajibu huo mzito.

“Ilipofika saa 6:00 usiku wa Desemba 9, tuliwasha mwenge tukio ambalo lilikwenda sambamba na kupandishwa kwa bendera ya uhuru wa Tanganyika katika Uwanja wa Taifa wa Uhuru jijini Dar es Salaam,” alisema Nyirenda katika moja ya mahojiano enzi za uhai wake.

Akisimika Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Tanganyika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro saa 6 usiku Disemba 9, 1961.

Brigedia Alexander Donald Gwebe- Nyirenda alikuwa mwanachama wa Rotary Club, mzee wa kanisa la Kipresbiteri la Mtakatifu Kolombas, na mwanachama wa Gideons International.

Alikuwa mcheshi na wote waliomfahamu watamkumbuka kwa hilo. Alikuwa mwanamichezo hodari na alicheza Squash na Golf, mbali na Raga amabayo aliacha kucheza akiwa na miaka 40 na soka- ambayo aliiacha akiwa na miaka 45.

Brigedia Nyirenda alifariki Desemba 20, 2008, majira ya saa 12:45. Ilibainika alikuwa anasumbuliwa na saratani ya umio kutoka Februari 2008, ugonjwa huo ulimdhoofisha hadi alipofariki kutokana na malaria kali.

Alimuoa Hilda Simkoko na walibarikiwa kupata na watoto 5 ambao ni pamoja na Marehemu Alexandra Katie Katinda, Suzyo Maimba Leziya, Atupiye Tima Hope, Alexander Nkutondwa Foti na Tiwonge Buchizga Andrew.