Historia ya maisha ya Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi

0
75

Ali Hassan Mwinyi alizaliwa Mei 8 mwaka 1925 katika kijiji cha Kivure, wilayani Kisarawe, mkoa wa Pwani na baadaye familia yake ilihamia Zanzibar.

Alisoma Shule ya Msingi Mangapwani kuanzia mwaka 1933 hadi 1936 kabla ya kujiunga na shule ya sekondari Dole mwaka 1937 mpaka mwaka 1942, na baadaye alijiunga na Chuo cha Ualimu Zanzibar kusomea ualimu kuanzia mwaka 1943 mpaka 1944.

Mwaka 1945 hadi 1950 alirejea katika Shule ya Mangapwani alikopata elimu yake ya msingi akiwa kama mwalimu, na kisha kupandishwa cheo na kuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo, wakati huo huo alikuwa akiongeza elimu yake kwa kujipatia General Certificate in Education (GCE) na pia aliendelea kusoma chuo cha Durban University Institute of Education, United Kingdom kusomea stashahada ya ualimu.

Baada ya hapo alijiunga tena na Chuo cha Ualimu Zanzibar kama mkufunzi kuanzia mwaka 1956 mpaka mwaka 1961. Pia alirudi Regent Institute kilichopo London nchini Uingereza ambapo alijipatia cheti cha ufundishaji lugha ya Kiingereza, kisha mwaka 1961 mpaka 1962 alijiunga na Hall University, Uingereza katika Tutors’ Attachment Course.

Safari yake ya kisiasa aliianza rasmi mwaka 1964 alipojiunga na Afro Shiraz Party (ASP) huko Zanzibar ambapo alikitumikia chama katika ngazi na nafasi mbalimbali. Kati ya mwaka 1964 na 1965 alikuwa katibu mkuu wa muda katika wizara ya elimu.

Majukumu mengine aliyokuwa nayo ni pamoja na Uenyekiti wa Zanzibar Censorship Board (1964-1965), Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na pia Mwenyekiti wa Baraza la Chakula na Lishe.

Kuanzia mwaka 1972 mpaka 1975, Mwinyi alikuwa Waziri wa Afya wa Tanzania kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuanzia 1975 mpaka 1977.

Mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri, cheo alichokitumikia mpaka mwaka 1982 aliporejea nyumbani na kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Rais wa Zanzibar wakati huo, Alhaj Aboud Jumbe mwaka 1984, Mwinyi alichaguliwa kuwa Raisi wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na wakati huo huo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuanzia Agosti mwaka 1984 Mwinyi alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, cheo alichoendelea nacho mpaka mwaka 1990 baada ya kung’atuka kwa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Rais Mwinyi aliingia madarakani na kuwa Rais wa Pili wa Tanzania kuanzia Novemba mwaka 1985 mpaka 1995.

Akiwa Rais wa Tanzania, ndipo nchi nyingi barani Afrika ziliingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa hapo ndipo jina la utani la “Mzee Rukhsa” lilipoanza, kwani Serikali ilianza kuruhusu mambo mengi kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa Tanzania pamoja na kukuza uhusiano na mataifa ya Magharibi.

Rais Mwinyi alikuwa akipatiwa matibabu tangu Novemba, 2023 London nchini Uingereza na baadaye kurejea nchini ambapo aliendelea na matibabu katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena, Dar es Salaam mpaka umauti ulipomkuta Februari 29, 2024.

Hayati Rais Mwinyi ameacha wake wawili (Sitti Mwinyi na Khadija Mwinyi) pamoja na watoto na wajukuu.

Send this to a friend