Hoja 9 walizobeba CHADEMA kwenye kikao na Rais Samia

0
49

Upatikanaji wa katiba mpya, tume huru ya uchaguzi, zuio la mikutano ya hadhara na makovu ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ni miongoni mwa hoja zilizobebwa na viongozi wa CHADEMA kwenda kwenye kikao cha Rais Samia Suluhu alipokutana na viongozi wa CHADEMA na CCM Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma Mei 20, 2022.

Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Tanzania Daima, hoja nyingine ambazo viongozi wa CHADEMA walikusudia kuwasilisha kwenye majadiliano hayo ni suala la wabunge 19 wa viti maalum, suala la ruzuku, usawa wa vyama vya siasa, watu waliochukuliwa hatua za kisheria kwa sababu za kisiasa na usalama wa wanasiasa waliokimbilia nje ya nchi.

Licha ya taarifa hiyo, Ikulu haijatoa taarifa yoyote kuhusu kilichojadiliwa na viongozi hao, lakini kwa kuzingatia vikao vya awali ambavyo Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alikutana na Rais Samia, bila shaka majadiliano hayo pia yalilenga kuimarisha demokrasia na hali ya kisiasa nchini.

Kwa upande wa CHADEMA kikao hicho kilihudhuriwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohammed, John Mnyika (Katibu Mkuu), na Katibu Mkuu wa BAWACHA, Catherine Ruge.

Ujumbe wa CCM ulimjumuisha Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka.

Send this to a friend