Hospitali ya Aga Khan Kenya yaamriwa kulipa faini bilioni 3 kwa uzembe
Mahakama Kuu nchini Kenya imeiamuru Hospitali ya Aga Khan kumlipa fidia ya zaidi ya Ksh.157 milioni [TZS bilioni 3.3] mke na mume kufuatia upasuaji wa kizembe uliofanyika mwaka 2006, na kusababisha madhara makubwa ya kiafya na kisaikolojia kwa mwanamke huyo.
Hospitali hiyo imepatikana na hatia baada ya daktari wa magonjwa ya wanawake, aliyefahamika kama mshtakiwa wa kwanza, kufanya upasuaji wa kuondoa mlango wa uzazi (cervix) bila idhini ya mgonjwa. Mwanamke huyo alikuwa ameridhia kufanyiwa upasuaji wa kuondoa mfuko wa uzazi na ovari pekee.
Jaji Muteti ameeleza kuwa kitendo hicho kilikuwa ni cha uzembe wa kiwango cha juu na ukiukwaji wa haki za msingi za mgonjwa. Ushahidi uliwasilishwa mahakamani kuwa hospitali ilimruhusu daktari huyo kufanya kazi licha ya kufutiwa leseni ya utabibu nchini Uganda kutokana na sababu za kiutumishi.
Mahakama pia imebaini kuwa hospitali ilishindwa kuweka vifaa muhimu vya uchunguzi, kama vile kifaa cha flexible cystoscope, hali iliyosababisha kuchelewa kugundua matatizo yaliyomletea madhara zaidi mgonjwa huyo.
Mwanamke huyo ameeleza mahakama kuwa alilazimika kusafiri hadi Afrika Kusini kwa matibabu ya kitaalamu kutokana na madhara aliyoyapata, jambo lililoongeza gharama kubwa ya matibabu. Aidha, alidai kupoteza uwezo wa kufanya kazi na kushuka kwa kiwango cha maisha, huku wakishindwa kufurahia maisha ya ndoa kikamilifu kutokana na athari za kimwili na kisaikolojia alizopata.