Hospitali ya KCMC yataja vipimo vya magonjwa 5 inavyotoa bure

0
51

 

Kuanzishwa kwa huduma za kibingwa bobezi katika hospitali hiyo na kuanzisha matibabu na uchunguzi wa saratani pamoja na ujenzi wa wodi ya wagonjwa wa saratani, kutapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro, hafla ambayo imeambatana na uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa jengo maalum la kutoa huduma za tiba ya Saratani kwa mionzi litakalogharimu TZS bilioni 4 litakapokamilika, ujenzi ambao unagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100.

Rais Samia amepongeza hospitali hiyo kwa kutoa huduma za vipimo vya sukari, macho, usikivu, shinikizo la damu na maradhi ya ngozi bila malipo na kutoa elimu ya UVIKO 19 pamoja na kutoa chanjo.

Aidha, amesema kuwekwa mashine za kisasa ikiwemo MRI, CT Scan, kuanzisha jengo la tiba ya Moyo, Figo na kutoa huduma za kibingwa kitapunguza rufaa ya wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi ambapo hivi sasa wagonjwa kutoka nje ya nchi wanakuja kupata huduma za matibabu hapa nchini na kuwezesha kufikia utalii tiba kama inavyokusudiwa.

Pia, ametoa wito kwa watafiti kuongeza wigo wa kuhakikisha idadi ya tafiti za magonjwa mapya na yale ya milipuko zinaisaidia Serikali kujipanga kukabiliana na majanga kwa kuandaa wataalamu pamoja na vifaa tiba vya kutibu magonjwa hayo.

 

 

Send this to a friend