Hospitali ya Muhimbili yapiga marufuku mifuko ya plastiki

0
14

Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili umepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki katika mazingira ya hospitali ikiwemo wodini na maeneo mbalimbali ya kutolea huduma kwa watoa huduma pamoja na ndugu wa wagonjwa.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma (MNH), Aminiel Aligaesha amesema katazo hilo linatolewa kufuatia uwepo wa mifuko ya plastiki kwenye mazingira ya hospitali iliyopigwa marufuku na Serikali.

“Mifuko hii inaletwa na baadhi ya ndugu wa wagonjwa ambao huitumia kama vibebeo vya chakula wanapokuja kutembelea ndugu zao waliolazwa wodini na baadhi ya watoa huduma hospitalini hapa,” amesema Aligaesha.

Aidha, kwa mujibu wa kiongozi huyo, katazo hilo linaanza mara moja na limelenga kampasi zote mbili za Hospitali ya Taifa Muhimbili ambazo ni Upanga na Mloganzila.