Hospitali ya Muhimbili yazindua mashine inayotibu magonjwa zaidi ya 10

0
70

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imezindua mtambo unaotumia hewa tiba yenye mgandamizo ya oksijeni (Hyperbaric Medicine Treatment) ambao unatibu magonjwa zaidi ya 10 na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na ya pili Kusini mwa Jangwa la Sahara kutumia mtambao huo uliogharimu TZS milioni 250.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mtambo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi amesema kupitia matibabu hayo, mgonjwa huingizwa kwenye kifaa maalumu na kupatiwa tiba kupitia hewa tiba ya oksijeni iliyogandamizwa kwa asilimia 100.

Amesema wagonjwa watakaonufaika ni wale wenye vidonda sugu ambavyo matibabu mengine yameshindikana kama wagonjwa wa sukari, walioathirika na moshi baada ya kuungua na moto na waliopata changamoto za upungufu wa oksijeni mwilini kama waliozama kwenye maji baharini nakadhalika.

Wagonjwa wengine ni pamoja na walioungua na moto, wenye upungufu mkubwa wa damu ambao kwa njia moja au nyingine hawawezi kuongezewa damu, waliopata ajali na kupata majeraha mwilini yasiyopona na wagonjwa wenye maambukizi kwenye mifupa isiyopona.

Ameongeza kuwa wagonjwa wengine waliopata mionzi na kusababisha sehemu zilizopata tiba mionzi kuathirika ikiwemo wenye saratani za koo, njia ya chakula na wale wenye tezi dume, waliofanyiwa upasuaji na kuwekewa/kupandikiziwa sehemu ya miili yao, wenye changamoto ya kusikia ambao vipimo vimeshindwa kuonyesha tatizo, wenye tatizo la usaha kwenye ubongo, wenye changamoto ya oksijeni kwenye mishipa ya damu na watoto wenye usonji.

Send this to a friend