Hotuba ya Mwenyekiti wa Chama Cha ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad kwa Wananchi wa Zanzibar kuhusu mlipuko wa Coronavirus, Jumamosi Aprili 4 2020

0
21

Ndugu Wananchi,

Naanza kwa kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kuturuzuku neema zake za uhai na uzima na siku ya leo na muda huu tukapata nafasi ya kuzungumza kupitia njia hii niliyoichagua.

Nakushukuruni na nyinyi kwa kuwacha shughuli zenu katika wakati huu mgumu na mkaamua kunisikiliza hapo mlipo.

Kwa sasa hapana asiyefahamu tena kwamba dunia imekumbwa na virusi vya COVID 19 maarufu kwa jina la Korona ambavyo vimesababisha na vinaendelea kusababisha maisha ya maelfu ya watu kupotea na shughuli za kila siku za uchumi kuvurugika. Nikiwa Kiongozi wenu mlionipa imani zenu nimeona ni muhimu sana kuzungumza nanyi moja kwa moja kuhusu namna ya kudhibiti na kuzuia maambukizi ya virusi hivi na hivyo kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu (Subhanahu Wa Ta’ala) kuokoa maisha yetu. Imekwisha elezwa kwa kina na wataalamu wa afya na kurudiwa na viongozi mbali mbali kuwa uwezo tulio nao sisi dhidi ya ugonjwa huu ni kujikinga na maambukizo na kuepuka kusambaza virusi kwa wengine. Hili ni moja ya jambo ninalotaka kulisisitiza katika hotuba yangu leo kwenu wananchi wenzangu.

Nchi yetu Zanzibar ni ya visiwa. Ni rahisi sana maambukizo kuingia nchini na kusambaa iwapo hatutakuwa makini. Lakini pia ni rahisi sana kuzuia maambukizo iwapo kila mmoja wetu atachukua jukumu na kutekeleza wajibu wa kujilinda na kulinda nchi yetu na watu wake tusipate maambukizo. Iwapo kila Mzanzibari atakuwa makini kuhakikisha kuwa hakuna mgeni anayeingia nchini bila kwanza kupimwa tutazuia virusi kuingia nchini kwetu. Hata hivyo, kama ambavyo mmesikia kuna watu tayari wameambukizwa virusi vya COVID 19 au Korona hapa Zanzibar. Vile vile, kuna watu wamewekwa karantini wakisubiri vipimo vyao kutoka maabara huko Dar es Salaam. Kwa hiyo, mbali ya kuwa walinzi dhidi ya watu kutoka nje ya Zanzibar, sote tunapaswa pia kuwa walinzi wa sisi wenyewe kwa wenyewe ndani ya nchi yetu kuzuia maambukizo ya virusi hivi.

Ndugu Wananchi,

Wataalamu wa maradhi ya Mripuko wanasema kuwa Virusi vya COVID 19 au Korona vinaambukiza kwa kasi kubwa kiasi kwamba mtu mmoja aliyeambukizwa anaweza kuambukiza wastani wa watu 3-5 katika hali ya kawaida tu bila mikusanyiko. Hivyo tunapoambiwa kuwa tuchukue tahadhari ya kukaa mbali na watu madhumuni yake ni kupunguza uwezekano wa watu kukutana na mtu mwenye maambukizo. Hatua hii ni muhimu sana kwa sababu kama watu hawakutani virusi havisambai. Ndio maana kupitia hotuba yangu hii kwenu, ninawaasa sana wananchi kuzingatia maelekezo haya na kuepuka mikusanyiko na kupunguza sana watu tunaokutana nao (kwa Kiingereza wanaita social distancing).

Ndugu Wananchi,

Naomba kurudia kwa ufupi maelezo ya wataalamu kuhusu dalili za ugonjwa wa Korona; ambazo ni pamoja na;

– Homa

– Kujisikia kuchoka

– Kichwa kuuma

– Kikohozi kikavu

Baadhi ya wagonjwa hupata maumivu, pua kuziba, kutoka kamasi, koo kukauka na hata kuharisha. Dalili zote hizi kuwa hazionekani sana na mara moja; bali huanza kidogo kidogo. Baadhi ya watu huambukizwa virusi vya Korona bila kuonesha dalili hizi lakini wanaweza kusambaza kwa wengine ambao wataonesha dalili hizi. Muhimu sana kuzingatia ni kuwa dalili hizi unaweza kuwa nazo lakini usiwe na virusi vya Korona kwa sababu ni dalili ambazo zinahusiana pia na maradhi mengine kama Malaria na hata ugonjwa wa Dengue.

Hivyo, ukiona dalili hizi usitaharuki, bali nenda Kituo cha Huduma za Afya kilicho karibu nawe kwa ajili ya kupata huduma ikiwemo kupata vipimo vya maradhi mengine, na kama itaonekana na wataalamu ni lazima, kuchukua vipimo vya Korona. Jambo muhimu sana nawasihi Ndugu Wananchi ni kujaribu kukaa mbali na watu uonapo dalili hizi ili kuepuka maambukizo iwapo watakuwa na Korona. Nawaomba sana msipuuze ushauri wa watalaamu kukaa umbali wa angalau mita mbili kutoka mtu na mtu. Hii ni kwa sababu mtu akikohoa au kupiga chafya na mtu huyo akiwa ameambukizwa virusi hivi ni rahisi mtu mwengine kuvuta hewa yenye virusi iwapo yupo karibu. Umbali wa Mita 2 unatosha kuzuia virusi kumfikia mtu mwengine.

Muhimu sana kuzingatia kuwa watu wazima kama mimi (wenye umri wa miaka 70 na zaidi) na wale wenye maradhi kama vile shinikizo la damu (yaani pressure), matatizo ya moyo, matatizo ya kifua, kansa na kisukari hushambuliwa zaidi na virusi vya Korona na kusababisha vifo vyao kwa haraka. Nawaomba sana wananchi muwalinde wazee wetu na wagonjwa kwa kutowakaribia sana kipindi hiki, kuwaepusha na misongomano ya watu na kuwafikisha kwenye vituo vya huduma za afya mara munapowaona wakiwa na hali ya homa, kukohoa na wakiwa wanapata shida kupumua. Tunaelekezwa na mafunzo ya dini kuwalinda wazee wetu. Nikiwa Kiongozi wenu nawaomba sana mzingatie maelekezo haya ili kuwaepusha wazee na wagonjwa dhidi ya maambukizo ya virusi vya Korona.

Hata na kwa vijana na wengineo wa rika zote, maradhi haya hayana kinga. Mwanadamu yeyote wa umri wowote ule ambaye ana athari nyengine ya kiafya (wataalamu wanaita underlying health condition or cause) basi pia hana usalama. Hata wewe ambaye unajihisi ni kijana na mzima wa afya basi hupo salama kama unavyofikiria. Hata kama Korona haitokuathiri wewe, basi ukishindwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya utakuwa ndani ya hatari ya kuwadhuru wenzako, marafiki, ndugu, jamaa, wazee, watoto, mke, au mume. Jiulize, utakwenda kusema nini mbele ya Muumba wako pale itakapodhihiri kuwa wewe ndiye uliyekuwa chanzo cha madhila na misiba ya wenzako? Tuchukue tahadhari na tufuate tunayoelekezwa.

Napenda kuwakumbusha namna ya kujikinga na maambukizi ya Korona ni:

– Kosha mikono yako mara kwa mara kwa maji na sabuni. Hii ni kwa sababu MAJI na SABUNI inaua vurusi vinavyoweza kuwa kwenye mikono yako.

– Kaa mbali na mtu mwengine kwa umbali wa mita 2 kwa sababu nilizoeleza hapo juu kuwa mtu akikohoa au kupiga chafya na akiwa karibu ni rahisi kuambukiza wengine au kuambukizwa.

– Jiepushe kushikashika macho, pua na mdomo wako. Hii ni kwa sababu mikono inaweza kugusa kitu chenye virusi na ukishika macho au pua au mdomo, virusi vitaingia mwilini mwako.

– Jiepushe kushikana mikono. Kwa sababu unaweza kushikana na mtu aliyeshika eneo lenye virusi na kukuambukiza.

Ndugu Wananchi,

Tukiyafuata haya kwa dhati tutaepusha uwezekano wa kuambukizwa virusi na kusambaza virusi kwa wengine. Kwa sababu hizi, ndio maana hata maeneo matakatifu ya Ibada kama vile Msikiti wa Makkah na Madina yamefungwa na hata HIJJA ya mwaka huu bado haijawa na uhakika kama itakuwepo kwa sababu ya kuepusha maambukizo. Vivyo hivyo, kwa wenzetu wa imani nyengine maeneo yao ya ibada pia yamefungwa. Nawaomba sana wananchi tuanze kufanya ibada majumbani kwetu katika kipindi hichi. Vile vile, tuna mila na silka zetu kama vile kukaa kwenye mabaraza na maskani nyakati za jioni kuzungumza masuala mbali mbali. Nakuusieni sana sana kuwa tuwache mikusanyiko hii wakati huu kwa sababu inaweza kuwa chanzo cha usambazaji wa virusi hivi.

Kwa namna ya pekee, naomba nizungumze na wanafunzi wetu, kwa maana ya vijana wetu na watoto wetu wanaosoma ambao kwa sasa mko majumbani kutokana na skuli, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu kulazimika kufungwa ili kuepusha uwezekano wa maambukizo ya virusi vya Korona. Mimi Kiongozi wenu nilikuwa Mwalimu kwa miaka mingi na nimesomesha wengi Unguja na Pemba. Ualimu ni kazi niliyoipenda sana na ndiyo iliyonifanya niitwe Maalim hadi leo. Kwa hivyo, nafahamu adha na machungu yenu na ya wazee wenu ya kukaa nyumbani na kukosa masomo. Lakini adha na machungu haya hatuwezi kuyaepuka ili kujiepusha na balaa kubwa zaidi. Ninachowanasihi ni kuutumia wakati wenu huu ambapo mko nyumbani kujisaidia wenyewe kwa kudurusu masomo yenu na kujitahidi kujiendeleza wenyewe hadi pale skuli, taasisi zetu za elimu na vyuo vikuu vyetu vitakapofunguliwa. Juweni kwamba Maalim Seif yuko pamoja na nyinyi.

Ndugu Wananchi,

Niliyoyaeleza mpaka hapa yanatuhusu sisi mmoja mmoja na kama jamii lakini natambua yapo mengine ambayo yanahitaji mamlaka kuchukua hatua iwapo kweli tumedhamiria kupambana na Korona na kuwanusuru wananchi. Kufunga mipaka ya bandarini na uwanja wa ndege ni hatua moja madhubuti. Lakini pia kuna haja kubwa na ya haraka ya kuanza kufanya Upimaji kwa Jamii (yaani public testing). Nitoe wito kwa mara nyengine tena kwa wenzetu Mashirika yote ya Kimataifa ya Afya watusaidie sana Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kuanzisha mifumo bora na ya haraka inayofaa ya kuwapima wale wote ndani ya jamii zetu hivi sasa walio katika hatari ya ugonjwa wa Korona. Nafahamu kuwa mifumo ya upimaji  hapa kwetu Zanzibar bado haijakaa vizuri. Hata maabara ya uchunguzi baada ya kuchukuliwa vipimo tunategemea ilioko Dar es Salaam. Lakini hatuna muda tena wa kupoteza. Mifano ya nchi za wenzetu waliofanikiwa kwa kiasi kikubwa hadi sasa kukabiliana na Korona imeonesha Upimaji katika Jamii (yaani Community Testing) ni msingi muhimu na mkubwa wa kupambana na adui huyu Korona.

Usafiri wa umma na hasa daladala nao ni hatari. Kuendelea kuachia watu bila ya mpango wowote thabiti wa kuelekea na kurudi kutoka kazini hususan katika Ofisi za Umma ni hatari nyengine. Nafahamu kuwa kuna mipango mbali mbali inafanywa hivi sasa kupunguza msongamano wa wafanyakazi katika Ofisi za Serikali. La kujiuliza ni kuwa ipo wapi Sera ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ya kuwashajiisha wanajamii kubaki majumbani na kuepuka misongamano au mikusanyiko isiyo na ulazima?

Ndugu Wananchi,

Kama ambavyo mnaona kwenye taarifa mbali mbali kutoka kote duniani, ugonjwa wa korona umeambukiza watu wengi sana na kusababisha vifo vya maelfu ya watu. Katika kila watu 100 waliopata maambukizo ya ugonjwa huu duniani, watu 5 wamepoteza maisha. Hapa kwetu Zanzibar, tumepewa taarifa ya wagonjwa 5 na kwa Tanzania nzima wamefika wagonjwa 20 huku mgonjwa mmoja akiwa amepoteza maisha. Naamini kuwa mmeona nchi kubwa kubwa duniani zinapoteza maelfu ya raia wao kutokana na kuzidiwa uwezo kwa mifumo yao ya afya na mahospitali. Ikiwa hali ni hivyo kwa nchi hizo tajiri zenye fedha nyingi sana, itakuwaje ugonjwa huu ukifikia hali kama hiyo katika nchi kama yetu? Mwenyezi Mungu Apishe mbali. Lakini Mfumo wetu wa Afya ni dhaifu sana, wataalamu wa afya ni wachache na vifaa vya huduma za afya havitoshi kabisa. Ni dhahiri kuwa nchi masikini duniani zinahitaji msaada mkubwa kutoka nchi tajiri ili kuweza kukabiliana na virusi vya Korona, kuokoa maisha ya watu na kuokoa shughuli za kiuchumi za watu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) tayari limeshaonesha wasiwasi wake mkubwa na hali ya kutisha itakayolikumba Bara la Afrika na sisi Zanzibar na Tanzania tukiwemo. Ndiyo maana mwezi huu wa Aprili ni mwezi muhimu sana utakaotupa viashiria vya hali njema au mbaya vya mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya Korona katika nchi za Afrika. Kwa Zanzibar na Tanzania kipindi hichi kitazidi kuwa kizito mno kabla ya hali kutengamaa.

Kufikia hapa, napenda pia kuzungumzia suala la kupanda gharama za maisha kipindi hichi na haja ya kudhibiti hali hii. Nakusudia upandishaji holela wa bei za bidhaa, kulindana katika utozwaji wa bei za bidhaa, ulipishwaji na utozwaji wa kodi kwa biashara zote zilizoathirika na zitakazoathirika na Korona, na mwenendo wa mamlaka zetu za kodi hasa TRA na ZRB. Huu ni wakati wa dharura ulimwenguni. Ni lazima hatua za dharura za kupunguza makali ya kiuchumi kwa wananchi zichukuliwe. Haiwezekani iwe sasa wakati huu ndiyo tunaanza kubinyana wakati tulichotakiwa tufanye ni kuwa na upendo wa kuwapunguzia wananchi mzigo wa gharama za maisha. Kila mmoja wetu anayejiita kiongozi ana wajibu wa kumlinda mwananchi maskini anayeteseka na kadhia hii.

Na kwa msingi huo, ndiyo maana ipo haja kubwa sana ya kujipanga kwamba iwapo tutafikia kipindi cha kuwataka watu wabaki majumbani (yaani Stay At Home), je tutawasaidia vipi wananchi kujikimu kwa angalau mahitaji yao ya msingi hasa chakula? Nalisema hili kwa sababu sote tunajua kuwa tunaelekea kunako msimu wa Mvua za Masika, Kipupwe na mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Naomba kuchukua nafasi hii pia kuvishukuru Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kujiandaa na kujidhatiti katika kutoa mchango wao mkubwa katika mapambano haya dhidi ya maambukizo ya virusi vya Korona, kama vinavyofanya Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya nchi nyengine. Papo hapo, nichukue nafasi hii kuviasa Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kuepuka kutumia nafasi zao vibaya. Mfano, ikiwa mamlaka hazijatangaza curfew kuanzia muda fulani hadi muda fulani au hazijatoa tangazo la wananchi kubaki ndani, inakuwaje baadhi ya askari wetu wachache kuwapiga na kuwaumiza vibaya watu wanaokutwa nje ya nyumba zao? Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vinawajibika kuwaongoza wananchi kwa upole isipokuwa pale tu ambapo kuna mtu mkaidi wa kupindukia, hapo askari wanaweza kutumia nguvu za wastani (reasonable force) zinazokubalika katika misingi ya sheria na zinazozingatia misingi ya haki za binadamu, na siyo nguvu za kupitiliza (excessive force). Nawanasihi sana Vyombo vyetu hivyo kuwa mfano katika kufuata sheria na kuonesha mapenzi na imani kwa wananchi wenzao hasa katika kipindi hichi kigumu tunachopitia.

Ndugu Wananchi,

Kwa miaka yote Bajeti za nchi zetu zimekuwa zikiweka pembezoni masuala yanayohusu huduma za afya. Tunapokumbana na miripuko ya maradhi kama ya Korona, kwa hakika uwezo wetu wa kukabiliana nayo unakuwa mdogo sana. Ubaya zaidi wa Korona ni kuwa shughuli zenu za kila siku zinaathirika. Hapa Zanzibar, theluthi moja ya Pato la Taifa inategemea Utalii na asilimia 80% ya mapato ya fedha za kigeni yanatoka kwenye Utalii. Korona imeua Utalii kabisa. Watu na hasa vijana waliokuwa wanategemea kuongoza Watalii ili kupata vipato vyao sasa hawana shughuli ya kufanya. Wafanyakazi wa mahoteli na mikahawa wapo nyumbani hawana kazi. Wasafirishaji wa Utalii kuanzia madereva wa taxi, prívate hire, daladala na hata marubani wa ndege za watalii sasa wapo nyumbani kwa sababu shughuli zimesimama. Hii pia inaleta changamoto kubwa kwa Mapato ya ndani ambayo yanategemewa kuwezesha Sekta ya Afya kufanya kazi. Kwa hali hii siyo tu kuwa Zanzibar itahitaji msaada kutoka Mataifa mengine, bali pia nchi zote zinazoendelea zitahitaji msaada mkubwa kutoka nje.

Takwimu za karibuni za Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN World Tourism Organisation) zinasema kuwa hata kama janga hili likiondoka leo basi tayari Soko la Sekta ya Utalii ulimwenguni kote lipo hatarini kuporomoka hadi Theluthi moja chini ya kiwango chake cha kawaida. Hii ina maana kuwa Anguko hili la asilimia 30% tayari limeshalipeka soko la sekta ya utalii katika athari ya muda mrefu na inaweza kuchukua mwaka au zaidi kurudi katika hali yake ya kawaida ya kabla ya janga la Korona. Kwa nchi za Visiwa kama ilivyo nchi yetu ambapo hivi sasa Utalii ndiyo nguzo ya uchumi wetu, athari hii ni kubwa mno kiuchumi na kijamii kuweza kuibeba.

Ndugu Wananchi

Ninatumia nafasi hii basi kuomba jamii ya kimataifa na hasa Mashirika na Taasisi za Fedha Duniani kusaidia Nchi zinazoendelea kwa kusimamisha kwa mwaka mmoja malipo ya madeni ili kutumia fedha zinazookolewa kujenga mfumo wa afya utakaoweza kusaidia watu masikini na pia kurejesha hali ya uchumi katika hali ya kawaida. Mataifa mengi hasa ya Afrika yanatumia fedha nyingi kuhudumia madeni yao, hasa madeni ya nje. Iwapo Taasisi kama Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (yaani World Bank na IMF), na vile vile nchi zilizoendelea zitasimamisha kutaka kulipwa riba ya madeni haya, nchi zetu zinazoendelea zitapata nafuu na hivyo kupata kwa fedha za kusaidia kukabiliana na virusi vya Korona na pia kusaidia shughuli za uchumi.

Ndugu Wananchi,

Tanzania ina Deni la Nje la jumla ya Dola za Marekani Bilioni 23 (sawa na shilingi Trilioni 53) ambapo asilimia 65% ya deni hili inatoka kwa Mashirika ya Kimataifa na Nchi Wahisani. Kiasi kilichobakia ni mikopo kutoka kwenye mabenki ya biashara. Iwapo wakopeshaji watakubali kusimamisha malipo ya deni kwa mwaka mmoja tu, basi Tanzania itabakia na Shilingi Trilioni 3 ambazo zitatumika katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi na kutoa msaada wa kulinda shughuli za biashara na uchumi ili kurejesha uchumi katika hali yake ya kawaida. Iwapo hili litafanyika, na Zanzibar ikapata mgao wake stahiki kutokana na nafuu hiyo, basi Zanzibar tutapata jumla ya shilingi bilioni 330 ambazo zitakuwa ni msaada mkubwa sana katika kujilinda na Korona na kuokoa uchumi wetu.

Ndiyo maana natoa wito kwa Mashirika ya Kimataifa kukubali kusimamisha Malipo ya Deni lao ili kuwezesha nchi zetu kukabiliana na mripuko huu ambao unaua watu na kuvuruga uchumi wa mataifa mbali mbali.

Ndugu Wananchi,

Namalizia hotuba yangu hii maalum kwenu kwa kuwanasihi sana kufuata maelekezo ya wataalamu ili kuzuia nchi yetu kupata maambukizo makubwa kwani uwezo wetu ni mdogo, hivyo ufumbuzi wetu ni KUJIKINGA. Kama kila Mzanzibari, bali na kama kila Mtanzania, atafuata maelekezo ya wataalamu wa afya kwa usahihi, tutapunguza maambukizo kwa kiasi kikubwa na kuushinda ugonjwa huu. Tukifanya uzembe, hospitali zetu, ambazo hali yake tunaijua wenyewe, hazitakuwa na uwezo wa kukabiliana na wingi wa wagonjwa na hivyo watu wetu wengi watapoteza maisha yao. Wito wangu kwenu, nikiwa Kiongozi wenu mnayenipenda na kunithamini – na mnatambua na mimi jinsi ninavyowapenda na kuwathamini – ni huo – TUJIKINGE.

Wakati nashirikiana na Viongozi wengine kushawishi jamii ya kimataifa kusaidiana nasi katika janga hili, nawaomba sana mzingatie maelekezo ya wataalamu – Nawa mikono kwa maji na sabuni, epuka kupeana mikono, epuka kujishikashika usoni, ziba uso unapokohoa au kupiga chafya, na zaidi epuka mikusanyiko.

Kabla sijamaliza, namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu Awape shifaa wote walioathirika na virusi vya Korona warudi katika hali ya uzima; na wale waliotangulia mbele ya haki Awajaalie makaazi yao yawe katika Pepo yake.

Nawatakia kila la kheri na salama katika mapambano haya. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, na kwa Umoja wetu na jitihada zetu za pamoja, tutashinda vita hivi na kurudi katika maisha ya kawaida. Mwenyezi Mungu Awabariki nyote.

Ahsanteni sana.

Send this to a friend