Hukumu ya Sabaya: Mafunzo matatu kwa wanasiasa vijana

0
16

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha leo imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya baada ya kutiwa hatiani katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Katika kesi hiyo iliyomhusisha Sabaya na waliokuwa walinzi wake wawili, Sylivester Nyegu na Daniel Mbura Februari 9 mwaka huu katika duka la Mohamed Saad walivamia na kufanya unyang’anyi wa zaidi ya TZS milioni 2.7 kwa kutumia silaha.

Kumekuwa na hisia tofauti mbalimbali kutoka mitandao ya kijamii kuhusu kesi hiyo iliyokuwa ikifuatiliwa kwa karibu sana tangu mwanasiasa huyo kijana alipokamatwa akikabiliwa na mashitaka mbalimbali.

Haya ni mambo matatu ambayo wanasiasa vijana kama Sabaya wanaweza kujifunza kutokana na hukumu hiyo:

1. Jinai inadumu
Haijalishi kosa la jinai limetendeka lini, wakati wowote mhusika angali hai anaweza kufikishwa mahakama kujibu tuhuma dhidi yake. Hili linadhidirika kwenye kesi ya mauaji ya aliyekuwa Rais wa Burkina Faso, Thomas Sankara ambapo miaka 34 imepita tangu mauaji hayo kutokea, lakini kesi hiyo imeanza kusikilizwa mwaka 2021. Watu 14 ambao walikuwa vijana wakati wa tukio hilo wanashikiliwa kwa kuhusishwa na mauaji hayo.

2. Jali maslahi ya umma
Katika kesi ya Sabaya na wenzake wamekutwa na hatia ya kuiba fedha za watu kwa maslahi binafsi. Ni muhimu kwa wanasiasa kujali maslahi ya umma na kuhakikisha matendo yao yanakuwa yenye kulenga kuboresha maisha ya watu aliowekwa kuwatumikia na sio kujinufaisha.

Kuna msemo wa kiswahili unaosema kuwa sauti ya wengi ni sauti ya Mungu au Mungu hatopuuza kilio cha wengi, hivyo hakikisha sauti ya wengi inayotolewa ni ya kuunga mkono yale unayoyafanya.

3. Madaraka ni koti la kuazima
Ni wazi ukiazima koti kuna siku mwenye nalo atalihitaji au utanyang’anywa. Pengine huenda ukataka kuliomba koti hilo kwa ngazi nyingine ya juu kutoka kwa wananchi kama diwani kwenda mbunge au mbunge kwenda Rais. Yote haya yatategemea ulipopewa koti hilo ulilitumiaje, na huo utakuwa ni wakati wa waliokupa koti hilo kufanya uamuzi.

Kwa ujumla, kila mmoja kwa nafasi yake katika kile anachokifanya anapaswa kuzingatia sheria, kanuni, miongo na maadili yanayoongoza utendaji wa anachokifanya.

Send this to a friend