Idadi ya laini za simu na matumizi ya intaneti vyaongezeka nchini
Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kumekuwa na ongezeko la laini za simu nchini hadi kufikia milioni 67.12 kutoka laini million 64.01 Juni mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.86.
Akitoa taarifa ya mwenendo wa Sekta ya Mawasiliano katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2023, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Jabiri Bakari amesema ongezeko hilo ni kutoka katika kampuni sita za simu nchini.
Aidha, amebainisha kuwa kwa upande wa intaneti, takwimu zinaonesha hadi kufikia Septemba mwaka huu kumekuwa na watumiaji wa intaneti takribani milioni 34.469 ikifananishwa na watumiaji ambao walikuwa milioni 34.047 Juni.
Ameongeza kuwa akaunti za pesa za mitandao ya simu zimeongezeka kutoka milioni 47.275 hadi milioni 51.36 Septemba ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.7, na kwamba katika ongezeko hilo, idadi ya miamala ya kifedha kwenye laini za simu imeongezeka kutoka milioni 420.6 katika kipindi cha Juni hadi kufikia milioni 422.36 Septemba.
Kwa upande wa visimbuzi vilivyokuwa hewani kwa Septemba vimefikia milioni 3.63 ikilinganishwa na visimbuzi milioni 3.34 mwezi Juni ambapo kati ya hivyo milioni 1.789 ni vya kidigitali yaani kwa mfumo wa DTT na milioni 1.8 ni mifumo ya satelaiti.