Ifahamu Homa ya Mgunda iliyoibuka Lindi, inavyoenea na namna ya kujikinga

0
39

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuwa upimaji wa sampuli za wagonjwa waliokuwa wakiugua ugonjwa usiojulikana katika Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi umethibitisha kuwa ni Ugonjwa wa Homa ya Mgunda (Leptospirosis, Field Fever).

Waziri Ummy amesema kuwa Homa ya Mgunda ni miongoni mwa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na unasababishwa na Bakteria aina ya Leptospira interrogans.

“Wanyama aina za panya, kindi, mbweha, kulungu, swala, na wanyamapori wengine wameripotiwa kupata maambukizi ya vimelea hivi na kuwa chanzo cha maambukizi kwa binadamu,” amesema waziri.

Amesema mtu anaweza kupata ugonjwa huo kwa kugusa mkojo (au maji maji mengine ya mwili) kutoka kwa wanyama wenye maambukizi; kugusa maji, udongo, au chakula kilichochafuliwa na mkojo wa wanyama wenye maambukizi au kunywa maji yaliyochafuliwa na vimelea vya bakteria wa ugonjwa huo huku maambukizi ya ugonjwa huu kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine hutokea kwa nadra.

Waziri Ummy amewataka wananchi kuchukua hatua zote stahiki za kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kuepuka kugusa maji au vitu vilivyochafuliwa na mkojo wa wanyama na kunywa maji safi na salama ambayo yamechemshwa au kutibiwa pamoja na kuwataka wagonjwa wenye dalili za homa, kuvuja damu, kichwa kuuma na mwili kuchoka kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili wapate matibabu sahihi.

Send this to a friend