
Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imetoa hati ya wito kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) na maofisa wengine watano kufika mahakamani kufuatia ombi lililowasilishwa na mawakili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Katika ombi hilo, mawakili hao wanaitaka mahakama iamuru Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche, afikishwe mahakamani au aachiwe kwa dhamana.
Akizungumza na Swahili Times, Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa CHADEMA, Wakili Gaston Garubindi amesema wengine waliotajwa kwenye hati ya wito ni Afisa Upelelezi wa Kanda Maalum Mkoa wa Dar es Salaam (ZCO), Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji.
Aidha, Wakili Garubindi amesema shauri hilo linatarajiwa kusikilizwa Novemba 07, 2025, saa 4:30 asubuhi katika Mahakama Kuu, Dar es Salaam.








