IGP Sirro apangua safu za makamanda wa polisi

0
46

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro amefanya uhamisho wa baadhi ya maofisa wa Polisi kwa lengo la kuboresha ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya jeshi hilo.

Baadhi ya maofisa waliohamishwa ni pamoja na Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) William Mkonda aliyekuwa Kamanda wa Polisi Tarime-Rorya, na sasa anakwenda kuwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZTO).

ACP Mkonda anakwenda kuchukua nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Abdi Isango ambaye anakwenda kuwa Mkuu wa Operesheni Mkoani Mbeya.

Aidha, IGP Sirro amemhamisha Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Zuberi Mwombeji ambaye alikuwa Mkuu wa Operesheni Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwenda Makao Makuu ya Polisi kuwa Mkuu wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii na Uchumi, huku nafasi yake ikichukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Kennedy P. Mgani ambaye alikuwa Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Mbeya.

Ofisa mwingine aliyehamishwa ni Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Pipi Kayumba kuwa Afisa Mnadhimu namba moja mkoani Singida, na nafasi yake kuchukuliwa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Tarcis Idelfonce aliyekuwa Mkuu wa Polisi wilaya ya Dodoma.

IGP Sirro amemhamisha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Jumanne Juke aliyekuwa Mkuu wa Polisi wilayani Geita na kuwa Mkuu wa upelelezi mkoa wa kipolisi Rufiji.

SSP Juke anachukua nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ame A. Anoqie ambaye amehamishiwa Tarime Rorya kuwa Afisa Mnadhimu namba moja, na kuchukua nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Geofrey B. Sarakikya ambaye anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa kipolisi Tarime Rorya.

Send this to a friend