IGP Sirro awaonya wanasiasa washari, asema wasilaumu vyombo vya dola

0
42

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro amewaonya vongozi wanaotoa matamshi makali na kuzungumza kwa ushari kuwa wasivilaumu vyombo vya dola endapo watachukuliwa hatua kutokana na matendo yao.

Akizungumza na ITV, IGP Sirro amewataka wanasiasa kutolichokoza jeshi hilo lakini wafanye kazi zao kwa utulivu na ushirikiano kuelekea uchaguzi mkuu wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

“Kwa kuwa nina dhamana ya ulinzi na usalama, wanaojiandaa kwa ushari wajue sisi tupo kwa mujibu wa sheria, na wanaozivunja sheria, tukianza kuwashughulikia wasitulaumu,” amesema Sirro.

Pia amewataka wananchi hasa vijana kutokubali kurubuniwa na kuingizwa katika vitendo vya uvunjifu wa amani au vitakavyohatarisha maisha na usalama wao.

Aidha, ameongeza kuwa Tanzania haiwezi kupata viongozi wazuri katika vurugu bali watapatikana kukiwa na amani tele na kwamba ni vyema viongozi hao wakaendelea kunadi sera zao kuliko kutafuta shari.

Send this to a friend