IGP Sirro: Hatuna taarifa za Tundu Lissu kutishiwa kuuawa

0
42

Jeshi la Polisi limesema halina taarifa ya madai yaliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kuwa ametishiwa kuuawa na watu ambao hawajajitambulisha.

Akizungumza na Gazeti ya Mwananchi, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro amesema kuwa mwanasiasa huyo hajatoa taarifa hiyo kwenye chombo cha usalama na wala hawana taarifa za yeye kukimbilia kwenye Ubalozi wa Ujerumani jijini Dar es Salaaam.

“Mimi nasikia kama ulivyosikia wewe. Muulize mwenyewe kama ameshawasiliana na chombo chochote cha usalama kama kuna shida hiyo,” IGP Sirro ameliambia gazeti hilo.

Sirro ameongeza kuwa wamesikia kwamba mwanasiasa huyo aliyegombea Urais wa Tanzania anahojiwa na Ubalozi wa Ujerumani, lakini hajasema chochote.

“Yeye anajua nipo, haji kunijulisha. Tunakutana naye katika magazeti. Si anatafuta hifadhi, sisi tutasemaje?”

Akizungumza na vyombo vya habari kwa nyakati tofauti Lissu amesema aliomba hifadhi ubalozini hapo tangu Jumatatu na kwamba ataendelea kukaa humo hadi hapo usalama wake utakapoimarika.

Lissu amedai kuwa alipigiwa simu na watu waliodai kuwa wameagizwa kummaliza na kwamba wakamtaka kama anaweza kujiokoa afanye hivyo.

Tukio la Lissu kuomba hifadhi katika ubalozi limezuia hisia tofauti miongoni mwa Watanzania kwani ni geni kwa wengine, huku wanazuoni wakisema kitendo hicho ni cha kawaida katika sheria za kimataifa.

“Ni kawaida kwa watu duniani kufanya hivyo wakiona mazingira yao ni hatarishi…” amesema Prof. Abdallah Safari

Mwanasiasa huyo alirejea nchini Julai 2020 baada ya kuwa nje nchi kwa takribani miaka mitatu akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi jijini Dodoma akiwa katika shughuli za kibunge.

Aligombea Urais kupitia CHADEMA na kushika nafasi ya pili baada ya kupata kura 1,933,271, akitanguliwa na Dkt. John Magufuli wa CCM aliyepata kura 12,516,252.

Send this to a friend